Rev. Kathy Kiuna: Kumtii mume wako si utumwa, ni utaratibu uliowekwa na Mungu

"Ninaelewa kwamba kwa ajili ya ndoa yetu kufanya kazi ipasavyo, sharti niwe chini ya mamlaka ya mume wangu," - Kathy

Muhtasari

• Kama mke ninaelewa kwamba mimi si duni kwa mume wangu, sisi pia tumeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu - Kathy.

Wanandoa ambao pia ni wachungaji Allan na Kathy Kiuna
Wanandoa ambao pia ni wachungaji Allan na Kathy Kiuna
Image: Instagram

Mchungaji wa kanisa la Jubilee Christian Church, JCC lililoko katikabarabara kuu ya Thika, Kathy Kiuna amewashauri wanawake kuwatii wanaume wao bila kuona kuwa wanaonewa wanapofanya hivyo.

Kathy ambaye ni mke wa mchungaji mwenza Allan Kiuna aliwausia wanawake walioko katika ndoa kutoona vibaya au kujihisi duni wanapofanya hivyo kwani ndio utaratibu uliowekwa na Mungu tangu siku za mwanzo wa dunia na kufanya hivyo ni kutekeleza wajibu.

Mchungaji huyo ambaye amedumu kwenye ndoa yake na mumewe kwa miaka 28 sasa aliendelea mbele na kunukuu Biblia kitabu cha Waefeso akisema kuwa kwa mwanamke yeyote ili kudumisha ndoa yake, ni sharti awe mtiifu kwa mumewe.

“Kila kitu ambacho Mungu aliumba kinafuata utaratibu uliowekwa awali, Hakuna jambo lolote ambalo Mungu hufanya ni la kubahatisha au fujo. Kuwa katika mpangilio haimaanishi kuwa wewe ni duni, inamaanisha unaelewa kuwa ili kitu chochote kifanye kazi vizuri, lazima kuwe na utaratibu.”

“Kama mke ninaelewa kwamba mimi si duni kwa mume wangu, sisi pia tumeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Lakini pia ninaelewa kwamba kwa ajili ya ndoa yetu kufanya kazi ipasavyo, ninajitiisha kwa hiari chini ya mamlaka ya mume wangu kwa kutii neno la Mungu katika Waefeso 5:22-23. Nguvu ya kweli hujaribiwa inapowekwa chini ya utiifu,” Mchungaji Kiuna alishauri.

Waanzilishi hao wa kanisa la JCC mwezi mmoja uliopita walisherehekea miaka 28 katika ndoa ambapo Kathy alimpiga busu Allan hadharani mbele ya umati wa waumini.

“Ni kumbukumbu ya miaka yetu na upendo wa maisha yangu. Ni vibe gani ya kufanya maisha na rafiki yangu bora. Tunapendana zaidi kuliko tulipoanza. Inaweza tu kuwa Mungu. Utukufu uwe kwa Mungu. @bishopkiuna nakulombotove,” Reverand Kathy Kiuna alisema.