KOT wamtupa mchekeshaji Njugush kwenye moto kisa kutangaza biashara ya benki

Mchekeshaji huyo alilazimika kuifuta video ile baada ya mashambulizi kuzidi.

Muhtasari

• Mwanzo, alifunga upande wa kutoa maoni lakini bado haikutosha na akaamua kuifuta.

• Hata hivyo, bado aliendelea kushambuliwa vikali kwa maneno yasiyo na huruma.

Njugush akiona cha mtema kuni Twitter
Njugush akiona cha mtema kuni Twitter
Image: Instagrma

Mchekeshaji Njugush alilazimika kufuta video yake kwenye Twitter baada ya kutupiwa mabomu ya kila aina na mashabiki wake.

Njugush alipakia video akiwa kwenye shule moja ya upili akipigia debe benki moja ya humu nchini, lakini maudhui yake yalipokelewa kwa njia hasi na mashabiki wake ambao walijikita Twitter na kuanza kumshambulia kwa cheche kali za kumdhalilisha.

Mchekeshaji huyo alikuwa amevalia sare za shule akizungumzia uzuri na faida za kutupia mfumo wa kulipa karo ya shule kupitia benki hiyo, lakini hili lilipokelewa tofauti na badala yake, akapokezwa maneno ya masimango, hadi kumpelekea kufuta video hiyo.

Hata hivyo, kuna baadhi ya walioipakua kabla ya kuifuta na waliitumia kumshambulia nayo huku wakisema aliotea vibaya mno kusukuma maudhui hayo.

“Huyu ni Njugush anajaribu kusukuma biashara ya benki kwa kutumia ucheshi wake, hata hivyo KOT hawakumpa nafasi na walijikita kwenye kipande cha kutoa maoni hadi akakifunga. Akiwa na wafuasi Zaidi ya milioni 2.1, hii ni mara ya kwanza kwa muda mrefu chapisho lake limeshindwa kufikisha hata likes elfu moja,” mmoja alisema.

“Njugush alifuta haraka video ya ucheshi na kufuatisha na machapisho ya vichekesho ili kuosha tangazo la awlai lakini haikufua dafu,” mwingine alisema.

Bado mchekeshaji huyo hajatoa tamko lolote kuhusu kilichotokea Twitter lakini mashambulizi dhidi yake yanaendelea kumuandama, wengi wakionekana kumtupia maneno kwa kile walisema alijaribu kuosha makossa ya benki hiyo kwa wateja wao.