Harmonize ni mzuri kukuliko, umeanzisha 'NEXT USHUZI' bila hela - Baba Levo kwa Rayvanny

Baba Levo ni chawa wa Diamond na katika chapisho hilo alimchokora Rayvanny ndani-nje bila huruma, alisema anamkubali Harmonize.

Muhtasari

• “Dogo bonge aling’ang’ania kutoka kwenye lebo, sasa kageuka omba omba kwenye casino,” Levo aliandika.

Baba Levo aanzisha vita na Rayvanny.
Baba Levo aanzisha vita na Rayvanny.
Image: Instagram

Wadaku na wambea wanahisi mambo si shwari baina ya wasanii Baba Levo na Rayvanny, baada ya chawa huyo wa Diamond kuibua madai ya ukakasi kwenye Instagram kumhusu Rayvanny.

Baba Levo kupitia Instastory yake alimchokora Rayvanny akisema kuwa alikurupuka kuondoka Wasafi bila kuwa na mipango dhabiti. Pia alisema kuwa Rayvanny siku hizi amekuwa omba omba kwenye klabu ya mcheza Kamari.

“Dogo bonge aling’ang’ania kutoka kwenye lebo, sasa kageuka omba omba kwenye casino,” Levo aliandika.

Katika tamko hili, wengi hawakuelewa alikuwa anamchamba nani, ila kupitia chapisho moja alilolifanya na kisha baadaye kulifuta, waliopiga picha ya ‘screenshot’ inaonesha moja kwa moja alikuwa anamshambulia Rayvanny.

 

Alisema waziwazi kuwa muda mwingine anamkubali sana Harmonize na jinsi anafanya mambo yake, kinyume na Rayvanny aliyemtaja kama aliyekurupuka kuondoka na kuanzisha lebo yake ya Next Level, ambayo Levo aliita Next Ushuzi.

“Kuna muda huwa namkubali sana Konde Boy. Ila si huyu dogo aliyekurupuka. Maisha yanahitaji utulivu sana. Ameanzisha Next Ushuzi wakati hana hela, bwana mdogo kawa mtu wa ajabu sana. Anavaa masweta makubwa anakuja kuomba. Kesho nitawaambia kuhusu mpaka hicho Kigali cha kufunua na kistudio chake,” screenshot hiyo ilisoma.

Haijabainika nini kinaendelea baina ya wasanii hao wawili ambao wamekuwa marafiki wa karibu hata baada ya Rayvanny kuondoka Wasafi.

Baba Levo amekuwa akimshambulia Harmonize kwa muda mrefu haswa muda ule alipotaka Rayvanny kukamatwa kwa kutoka kimapenzi na Paula Kajala, alitoa wimbo wa kumtukana Harmonize, lakini cha ajabu safari hii alionesha kumkubali.