Diamond atumia nguvu nyingi kuomboleza Costa Titch, mbona hakufanya hivo kwa AKA?

Video zinazosambaa mtandaoni zinaonyesha nyota huyo wa Amapiano akianguka mara mbili jukwaani wakati wa onyesho Johannesburg.

Muhtasari

• Baadhi walizua kwamba Diamond ana ubaguzi dhidi ya sehemu ya wasanii wa Afrika Kusini kwa kutomuomboleza AKA na kufanya hivyo kwa Titch.

Diamond amuomboleza Costa Tirch, mbona hakufanya hivyo kwa AKA?
Diamond amuomboleza Costa Tirch, mbona hakufanya hivyo kwa AKA?
Image: Instagram

Wikendi iliyopita, mashabiki na wapenzi wa muziki wa Amapiano kutoka Afrika Kusini kwa mara nyingine tena walitupwa kwenye dimbwi la maombolezo kufuatia kifo cha ghafla cha rapa Costa Titch.

Mashabiki mbalimbali wa msanii huyo pamoja na wasanii wenzake walijitosa kwenye mitandao ya kijamii kumuomboleza na kusimama na jamii ya wanamuziki Afrika Kusini kwa maombolezo, chini ya miezi miwili tu baada ya kifo cha utata cha rapa mwingine, AKA.

Afrika Mashariki, msanii Diamond alimuomboleza Titch kama rafiki wa dhati kwa kupakia msururu wa picha kadhaa za msanii huyo.

Diamond hata hivyo hakuishia hapo, alifanya tukio kubwa kabisa ambapo alibadilisha picha ya utambulisho wake Instagram na kupakia ile ya Titch kama njia moja ya kumuenzi kwa urafiki uliokuwa mzuri enzi za uhai wake.

Hata hivyo, tukio hili kutoka kwa Diamond lilipokelewa kwa njia tofauti, baadhi wakirejelea kifo cha AKA wiki chache zilizopita.

Ikumbukwe kwamba wakati AKA alifariki kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana waliomvizia kwenye mgahawa, wasanii wengi walimuomboleza kwa kupakia picha yake lakini Diamond hata hakuonekana kuguswa na msiba huo – kwani hakupakia picha yake wala kuandika maneno yoyote ya kumuomboleza licha ya kufanya collabo moja mwaka 2016 na AKA.

Baadhi walizua ngonjera zao kuwa Diamond ana ubaguzi wa wasanii wa Afrika Kusini ambapo mara kwa mara anafanya ziara zake za kula bata, wakionekana kuhoji mbona Titch na mbona hakufanya hivyo kwa AKA.

Kwa hiyo Asake Wa Tandale ana ubaguzi kwa baadhi ya wasanii aliofanya nao kazi? Mbona rapa AKA alivyofariki Diamond hakupost chochote? .. Kiki tu hamna lolote Fyuuuuu” Mmoja kwa jina DJ Amani alilalamika.

Jamaa kamuweka dp coz marehem amefanya nyimbo 4 kunako kundi la wcb moja ni fresh, shetani moyo na superstar,” Paul Ezra alifafanua.

Costa Titch alianguka na kufa wakati wa onyesho la moja kwa moja huko Johannesburg. Rapa huyo ambaye jina lake halisi ni Constantinos Tsobanoglou alikuwa akitumbuiza kwenye tamasha la Ultra Music Festival.

Video zinazosambaa mtandaoni zinaonyesha nyota huyo wa Amapiano akianguka mara mbili jukwaani wakati wa onyesho hilo. Rapa huyo alifahamika sana kwa wimbo wake wa Big Flexa ambao ulimfanya apate umaarufu. Hadi sasa wimbo huo umetazamwa zaidi ya mara milioni 45 kwenye YouTube.