Mike Sonko apigwa na butwaa kugundua marafiki zake ambao ni wanachama LGBTQ

Sonko alifichua kwamba amegundua baadhi ya marafiki zake walikuwa katika serikali ya rais mstaafu Uhuru Kenyatta.

Muhtasari

• Sonko alisema marafiki hao wanamtaka kukomesha harakati hizo kwani ughaibuni ni jambo halali kisheria.

• Jumatano, Sonko alipoteza ukurasa wake wa Facebook wenye wafuasi milioni 2.5 kwa kushambulia LGBTQ.

Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko
Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko
Image: Facebook// Mike Sonko

Mfanyibiashara na mwanasiasa Mike Sonko ni mtu mwenye mashaka na wasiwasi mwingi. Hii ni baada ya kugundua kwamba baadhi ya marafiki zake ni wanachama shakiki katika jumuiya ya wapenzi wa jinsia moja, LGBTQ.

Sonko ambaye Jumanne alitangaza kufungiwa kurasa zake za mitandao ya kijamii inayomilikiwa na kampuni ya Meta, ikiwemo Facebook amekuwa akitumia mtandao wa Twitter kuendeleza harakati zake dhidi ya LGBTQ.

Anasema kwamba baadhi ya marafiki hao wake ambao ni wanachama wa LGBTQ wamekuwa wakimpigia simu tangu jana wakimtaka kukoma kuendeleza harakati hizo kwa kile walimwambia kwamba hata ughaibuni, LGBTQ imehalalishwa kisheria kwa hiyo harakati zake zitaenda tu na maji – kazi bure!

Hata hivyo, Sonko ambaye aliapa kutolegeza Kamba katika kampeni zake dhidi ya LGBTQ alifichua Zaidi kwa mshangao mkubwa kwamba baadhi ya hao marafiki zake walikuwa katika serikali iliyopita iliyokuwa ikiongozwa na rais mstaafu Uhuru Kenyatta.

“Wawawaaaaa!! Kumbe mpaka marafiki zangu baadhi yao ni mashoga hata wake walikuwa kwa serikal iliyopita. Huwezi amini wananipiga simu wanasema tuwachane na hiyo stori ya LGBTQ ati uko ughaibuni iko mpaka kwa sheria. Je, una maoni gani kuhusu hili?” Sonko aliuliza kwa kuchanganyikiwa.

Jumatano, Sonko alifungiwa ukurasa wake wa Facebook wenye wafuasi Zaidi ya milioni 2.5 na kutakiwa kuomba radhi jamii ya LGBTQ kabla ya kuandika barua ya kutaka kurudishiwa ukurasa huo.

Hata hivyo, mwanasiasa huyo ambaye katika siku za hivi karibuni amekuwa akishambulia LGBTQ kwa kuchapisha video na picha za watu wanaodhaniwa kuwa wanachama wake aliapa kuwa hatoomba msamaha wala kuandika barua ya kutaka kurudishiwa ukurasa huo.

Alisema ataendeleza mashambulizi yake kupitia mtandao wa Twitter ambao ni mshindani mkubwa wa Meta, mmiliki wa Facebook katika soko la mitandao ya kijamii.