Bahati kumnunulia mkewe Diana Marua nyumba Dubai?

“Mimi nataka tu nyumba ya kuja kupumzika hapa ... kupumzika na kujivinjari. Je, ni mengi sana kuuliza, mpenzi? nifurahishe" - Diana.

Muhtasari

• Wapenzi hao wawili wapo jijini Dubai kwa ziara ya kujifurahisha ambapo pia wamepata ubalozi wa kutangaza utalii wa jiji hilo.

Diana Marua amtaka Bahati kumnunulia nyumba Dubai
Diana Marua amtaka Bahati kumnunulia nyumba Dubai
Image: Instagram

Msanii Bahati Kioko amedokeza kwamba huenda tena akamnunulia mkewe Diana Marua nyumba ya kifahari katika jiji la Dubai kama zawadi ya kumshukuru kwa kumzalia watoto watatu wazuri.

Bahati na Diana wako jijini Dubai ambapo wametangaza kutia kibindoni dili la ubalozi wa utalii wa Dubai wakiwakilisha ukanda wa Afrika ya Kati na Mashariki.

Wakiwa katika ufuo mmoja wa bahari kwenye madhari mazuri, Bahati alidokeza kwamba huenda akaingiwa na vishawishi visivyoweza kuepukika kumnunulia Marua nyumba katika jiji hilo la kifahari duniani.

Hata hivyo, ni swali alilouliza kwa wafuasi wake akitaka maoni yao kama amnunulie Marua nyumba au asubiri kiasi kwanza mkewe atosheke na jumba alilomnunulia mwaka jana kama zawadi ya Valentino.

“Diana anataka nimnunulie nyumba mpya katika jiji la Dubai, nifanye hivyo ama atulie kwanza kwa ile ya kifahari niliyomnunulia Kamakis?” Bahati aliuliza.

Kwa upande wake, mkewe Diana Marua alimjibu akisema kwamba ije mvua lije jua anataka kununuliwa jumba la kifahari katika jiji hilo la Miliki za Kiarabu, akitaja madhari yake kuwa pendwa kwake.

“Mimi nataka tu nyumba ya kuja kupumzika hapa ... kupumzika na kujivinjari. Je, ni mengi sana kuuliza, mpenzi? @bahatikenya nakupenda Dzaaaaaddyyyy... nifurahishe,” Diana alimwambia Bahati.

Bahati waliondoka nchini siku mbili zilizopita wakisema walikuwa na ziara ya kujiburudisha nje yqa nchi, lakini Jumatano waliweka wazi kwamba walifanikiwa kupata dili la kuwa mabalozi wa kuutangaza utalii wa Dubai kote nchini, wakiliwakilisha taifa la Kenya na ukanda huu kwa jumla.