Nilinyimwa haki za kutumia picha za mwanangu kuunda filamu ya kumkumbuka - mamake Kanumba

Kuna mmoja nilimuomba kutumia picha za Kanumba kwenye filamu ya kumbukumbu za Kanumba, hakuwa tayari kunipa ushirikiano" - Bi Mutegoa.

Muhtasari

• Alisema kwamba Kanumba alikuwa anauza hakimiliki zote za kazi yake mpaka moyo wake, jambo ambalo limefanya kuwa vigumu yeye kupata mapato ya kazi zake.

Mamake Kanumba alia kutopata mapato kutoka kwa filamu za mwanawe.
Mamake Kanumba alia kutopata mapato kutoka kwa filamu za mwanawe.
Image: scrweengrab, maktaba,

Steven Charles Kanumba, ni jina ambalo huwezi kosa kulitaja wakati unazungumzia simulizi ya filamu za Kitanzania, maarufu Bongo Movie.

Ni mwigizaji nguli aliyefufua na kubeba tasnia ya filamu za Bongo mabegani mwake kwa ufanisi mkubwa kwa Zaidi ya miaka 7, kabla ya mkono katili wa umauti kumnyakua ghafla mwaka 2012.

Mpaka kifo chake, Kanumba alikuwa ameitangaza Sanaa ya uigizaji ya Tanzania ndani na nje ya taifa hilo hadi kufanikiwa kuwa mwigizaji wa kwanza aliyeshirikiana na Wanaigeria katika kufanya filamu ambayo ilitazamwa na wengi.

Kwa mafanikio makubwa, alianzisha kampuni ya kuzalisha filamu, 'Kanumba The Great', ambayo alipofariki ilibaki mikonono mwa mama yake, Flora Mutegoa.

Katika mahojiano ya wikendi na blogu moja, Bi Mutegoa alizungumza kwa uchungu kwamba licha ya mwanawe kuacha filamu nyingi pendwa ambazo mpaka leo hii hazijawahi isha ladha, yeye kama mama yake hajawahi pata posho lolote kutokana na usambazaji na uuzwaji wa filamu hizo.

Bi Mutegoa alidai kwamba Kanumba alikuwa amepeana hakimiliki zote za filamu, hali ambayo ilimfanya hata kipindi kimoja akijaribu kutengeneza filamu ya kumbukumbu za Kanumba, kufungiwa haki za kutumia picha za mwanawe katika filamu hiyo ya kumbukubmu za mwanawe.

“Kwa bahati mbaya, wakati Kanumba anafanya kazi zake, alikuwa anauza kila kitu, mpaka yaani na roho yake. Kwa hiyo mimi sina haki yoyote ya ile kazi ya Kanumba. Wanaofaidika ni wale. Na kwa bahati mbaya wengine hata hofu ya Mungu hawana, kuna mmoja nilimuomba kutumia picha za Kanumba kwenye filamu ya kumbukumbu za Kanumba, hakuwa tayari kunipa ushirikiano,” Bi Mutegoa, mamake na marehemu Kanumba alisema kwa mfadhaiko mkubwa.

Bi Mutegoa alisisitiza kwamba hakuna kazi ya Kanumba hata kidogo inayomfaidisha Zaidi ya kubaki na kampuni tu.

Alisema kwamba suala hilo limekuwa likimkosesha usingizi sana na kipindi kimoja serikali ya awamu ya tatu ilimsimamia mpaka moja ya kampuni zinazosambaza kazi za filamu za Kanumba kwa jina ‘Steps’ kumlipa hakimiliki kidogo, lakini makampuni mengine hata senti tano hajapata kuiona.