"Kuna wakati wa kila kitu" Davido amalizia kumuomboleza mwanawe, arudi kwenye muziki

Mwimbaji huyo alitoa shukrani za dhati kwa wote ambao walisimama naye.

Muhtasari

•Katika taarifa yake kwenye mtandao wa Instagram siku ya Jumanne, staa huyo wa Afrobeats alibainisha kuwa kila jambo lina wakati wake. 

•Wakati huohuo, alitangaza kwamba ataachia albamu yake mpya 'Timeless' mwishoni mwa mwezi Machi.

Davido alikuwa na mwanawe Ifeanyi na mpenzi wake Chioma Rowland miaka mitatu iliyopita
Image: BBC

Mwimbaji wa Nigeria David Adedeji Adeleke almaarufu Davido ametangaza mwisho wa kipindi cha kumuomboleza mwanawe Ifeanyi Adeleke.

Katika taarifa yake kwenye mtandao wa Instagram siku ya Jumanne, staa huyo wa Afrobeats alibainisha kuwa kila jambo lina wakati wake. 

"Kuna wakati wa kila jambo. Wakati wa kuomboleza na wakati wa kupona. Wakati wa kucheka na wakati wa kucheza Wakati wa kusema na wakati wa kunyamaza," alisema.

Mwanamuziki huyo alitumia fursa hiyo kutoa shukrani za dhati kwa wote ambao walisimama naye katika kipindi kigumu cha kumuomboleza mwanae.

"Upendo wote na jumbe nilipokuwa mbali, zawadi zilizotumwa, matamasha ambayo ninyi nyote mlifanya! Ninashukuru kwa yote. Leo, nataka kuwakumbusha wote kwamba kile ambacho sasa hakina wakati, kilikuwa kipya, ni wakati wa mpya," alisema.

Wakati huohuo, alitangaza kwamba ataachia albamu yake mpya 'Timeless' mwishoni mwa mwezi Machi.

Mwanawe Davido, Ifeanyi Adeleke, alikufa maji kwenye kidimbwi cha kuogelea nyumbani kwake  katika jiji la Lagos, Nigeria mnamo Oktoba 31, 2022. Taarifa kuhusu kifo cha mvulana huyo wa miaka mitatu zilishtua, si familia ya mwanamuziki huyo pekee bali pia mamilioni ya mashabiki wake kote duniani. 

Wiki jana, mwanamuziki huyo alifuta picha zote kwenye ukurasa wake wa Instagram na kubakisha machapisho 3 tu!

Machapisho matatu ambayo aliyabakisha ni lile la picha ya mtoto wake marehemu ambayo alipakia kumsherehekea mnamo siku yake ya kuzaliwa siku chache kabla hajafa, ya pili ikiwa ni ya pamoja akiwa na mkewe Chioma jukwaani na chapisho la tatu likiwa la picha ambazo alipigwa akitumbuiza jukwaani katika hafla ya kufunga mashindano ya kombe la dunia Qatar mwezi Desemba.

Davido ambaye alikuwa amesalia kimya tangu alipompoteza  mwanawe alikuwa akipitia wakati mgumu sana wa kukubali kifo hicho, kulingana na wandani wake.