"Kutembea, kuongea ni shida" Mc Fullstop atoa taarifa ya wasiwasi kuhusu afya yake iliyodhoofika

Pafu langu la kushoto limeanguka kabisa nimebaki na moja," alisema.

Muhtasari

•Maina alifichua kuwa pafu lake moja limeathirika kabisa baada ya kuugua ugonjwa wa Kifua Kikuu kwa muda mrefu.

•Alidokeza kwamba hajisikii sawa na kuwashukuru wale ambao wamekuwa wakisimama naye wakati wa ugonjwa wake.

Mc Fullstop
Image: HISANI

Mtangazaji mashuhuri wa Reggea, John Maina almaarufu MC Fullstop ametoa taarifa ya kuhuzunisha kuhusu afya yake inayozidi kuzorota.

Akizungumza kwenye kurasa zake rasmi za mitandao ya kijamii siku ya Jumatano asubuhi, Maina alifichua kuwa pafu lake moja limeathirika kabisa baada ya kuugua ugonjwa wa Kifua Kikuu kwa muda mrefu.

Mtangazaji huyo maarufu wa nyimbo za Reggea na Dancehall alibainisha kwamba kwa sasa anapata shida sana kukimbia, kutembea na hata kuzungumza baada ya ugonjwa huo kuathiri mapafu na koo lake.

"Hii imeenda” kwa kweli. Pafu langu la kushoto limeanguka kabisa nimebaki na moja," alisema kwenye ukurasa wake wa Facebook.

Aliongeza, "Mwaka wa 2021 niligunduliwa na TB ya mapafu ikakula mapafu kabisa. 2022 nikapata TB ya koo nayo ikanimaliza sauti. Kukimbia, kutembea na kuongea ni shida,"

Maina aliambatanisha ujumbe huo na picha yake akiwa amelala kwa kitanda cha hospitali huku akiwa anawekwa hewa kupitia mrija ambao uliwekwa kwenye pua lake na picha nyingine ya X-ray iliyoonyesha jinsi pafu lake limeathirika.

Alidokeza kwamba hajisikii sawa na kuwashukuru wale ambao wamekuwa wakisimama naye wakati wa ugonjwa wake.

"Alafu mapafu yana ufala sio kama ini, haiwezi kujiponya itabidi nijipange hapa naona niki hang boots. Nataka tu kusema asante kwa wale wamekuwa wakinisapoti katika kipindi hiki kigumu Mungu awabariki sana," alisema.

Mapema mwezi huu, mtangazaji huyo mahiri alighairi shoo aliyotazamiwa kutumbuiza mjini Nakuru baada ya kulazwa hospitalini.

Katika taarifa yake, Maina aliwaomba radhi mashabiki wake kufuatia tukio hilo lisilotarajiwa na kuwaomba waendelee kumsapoti.

"Tunaomba sapoti na kuelewa kwenu katika kipindi hiki kigumu. Asanteni kwa sapoti yenu inayoendelea, na ninatumai nyote mtajitokeza kwenye shoo," alisema kupitia taarifa mnamo Machi 15.

Maina ambaye anatambulika kwa jina la kisanii ,MC Fullstop, anajulikana sana kwa matangazo yake ya kusisimua ya Reggea katika vilabu na televisheni.