Ni upuzi watoto kuacha shule kisa wana umaarufu mitandaoni - Jaymo Ule Msee ashauri

Mcheshi huyo alisema watoto wengi wakishapata umaarufu TikTok, wanaingiwa na fikira ya kuacha shule wakidhani umaarufu utawalipa.

Muhtasari

• Jaymo alisema kuna tofauti kubwa kati ya kuwa maarufu na kuwa mshawishi.

• Mchekeshaji huyo alisema ushawishi ndio kazi kubwa na ndio hulipa watu lakini umaarufu haujawahi lipa mtu.

Jaymo Ule Msee atoa tofauti kati ya kuwa maarufu na kuwa na ushawishi mitandaoni.
Jaymo Ule Msee atoa tofauti kati ya kuwa maarufu na kuwa na ushawishi mitandaoni.
Image: Instagram

Mchekeshaji Jaymo Ule Msee amesema mitandao ya kijamii imeharibu uhalisia wa mambo mengi ambayo alisema watu wengi wanafanya visanga na ‘masinema’ ili kutafuta umaarufu kuliko kufanya vitu vya ukweli.

Alisema kuwa watu wengi wanataka kupata ufuatiliaji mkubwa kwenye mitandao ya kijamii wakiamini kwamba huo ndio umaarufu ambao utaanza kuwaingizia kipato.

Mchekeshaji huyo ambaye pia ni mtangazaji katika kituo kimoja cha redio humu nchini alikosoa dhana hiyo, akisema kwamba watu haswa vijana wanafaa kuelimishwa kuhusu umaarufu wa mitandaoni na maisha ya uhalisia.

“Mitandao ya kijamii imekuja na masinema. Ukiona sinema, chunguza sana. Ndio maana mimi napenda kuangalia filamu kwa sababu najua hawa watu wanaigiza. Hivyo ndivyo vitu vinafanya watoto pale chini kutaka umaarufu wakidhani ni mafanikio,” Jaymo alisema.

Mchekeshaji huyo pia alisimulia kisa cha mtoto aliyeacha shule kidato cha pili akiamini kuwa atapata kipato kutokana na kuwa na ufuatiliaji mkubwa TikTok.

“Kuna msichana wa kidato cha pili ameacha shule eti kwa sababu anajulikana sana TikTok akiwa na wafuasi elfu 67. Kwa hiyo anaamini kwamba yeye ni mshawishi mkubwa. Unapata yule mtoto anafikiria yeye ni staa na anafaa kulipwa kwa ile mitikasi anafanya TikTok,” Jaymo alisema kwenye podiskasti ya Iko Nini.

Alitoa tofuati iliyopo baina ya kuwa maarufu mitandaoni na kuwa mshawishi wa kuvutia mapato.

“Kuwa mshawishi, ni ufanye kitu, ili sisi tununue, na kuwa na umaarufu ni kwamba mtu Fulani anajulikana sana. Ushawishi ndio hufanya watu walipwe, lakini umaarufu sijawahi ona ukilipa watu.”