Paula amdhihaki Rayvanny baada ya kurudiana na Fahyma, akiri kumpenda Marioo

Mwanamitindo huyo mrembo alikiri kujuta kutokutana na Marioo awali.

Muhtasari

•Jumamosi, Marioo alisifu urembo wa mwanamitindo huyo mwenye umri wa miaka 20 na kubainisha kuwa anampenda.

•"Natamani ningekutana nawe awali," Paula alimwambia Marioo.

Paula Kajala, Rayvanny, Marioo
Image: HISANI

Inaonekana mwanamitindo Paula Kajala yuko tayari kuweka kinyongo baada ya aliyekuwa mpenziwe, Rayvanny kurudiana na mzazi mwenzake Fahyma na hata kumshirikisha katika video ya wimbo wake mpya wa ‘Forever.

Katika siku kadhaa za hivi majuzi, Paula ameonekana akijivinjari na staa mwingine wa Bongo, Omary Mwanga almaarufu Marioo na kumekuwa na vidokezo kuwa atashirikishwa kwenye video ya wimbo ijayo wa mwanamuziki huyo.

Haijabainika iwapo wawili hao wanatoka kimapenzi lakini kwa hakika wamekiri kupendana. Siku ya Jumamosi, Marioo alisifu urembo wa mwanamitindo huyo mwenye umri wa miaka 20 na kubainisha kuwa anampenda.

"Imagine mtoto mbichi kama huyu alafu anakupenda.. @therealpaulahkajala #ananipenda inakuja hivi karibuni," Marioo aliandika chini ya video ya Tiktok ya Paula akicheza wimbo wake mpya 'Ananipenda.' 

Huku akijibu kwenye chapisho hilo la Instagram, binti huyo wa muigizaji Kajala Masanja alisema laiti wangekutana awali.

"Natamani ningekutana nawe awali," aliandika na kuambatanisha na emoji zilizoashiria mahaba mazito kwake.

Marioo aliendelea kumtambua mwanamitindo huyo kama kipenzi chake.

Matukio haya yanajiri takriban wiki moja tu baada ya Rayvanny na Fahyma almaarufu Fayvanny  kuthibisha kufufuka kwa mahusiano yao yaliyosambaratika takriban miaka mitatu iliyopita. Hii ni ya bosi huyo wa Next Level Music kumshirikisha mzazi huyo mwenzake katika video ya wimbo wake mpya 'Forever.'

“Mtoto mbichi teketeke aki Mama umelainika. Umeumbika, acha nikumwagie sifa. Waruke sakara na mateke uzuri wako hawatofika, mama umejazisha, mikate ya kumiminisha,” Rayvanny alimsfia Fahyma kwenye wimbo huo.

Takriban siku mbili baada ya kuachia wimbo huo, bosi huyo wa Next Level Music alithibitisha kuwa sasa hata wanaishi pamoja.

Rayvanny na Fahymah walitengana mwaka wa 2019 ambapo kila mmoja aliamua kuenda njia yake. Baada ya kutengana, haikumchukua Rayvanny muda  mrefu kabla ya kuzama kwenye huba zito na bintiye Kajala, Paula Paul.

Hata hivyo, mwaka jana, bosi huyo wa Next Level Music alidokeza kuvunjika kwa mahusiano yake na mwanamitindo huyo wakati akitumbuiza katika tamasha la Fiesta 2022 mjini Sumbawanga, Tanzania.

"Mapenzi yasikuchanganye nakwambia, usije ukapata bila kama Dulla. Mapenzi usije kufananisha,  kama  vile chakula. Nilinyosha moyo Karula, nikaachana na Paula..." aliimba.

Mapema mwaka huu alidokeza kujuta kuvunjika kwa mahusiano hayo, na baadaye kidogo akadokeza kurudiana naye.

Mwezi Februari, Rayvanny alichapisha picha ya binti huyo wa muigizaji  Frida Kajala Masanja na chini yake kuambatanisha na emoji za moyo wenye moto, ambazo kwa kawaida hutumika kuashiria mapenzi.

"❤️‍🔥❤️‍🔥❤️‍🔥❤️‍🔥,"  aliandika kwenye picha nzuri ya kipusa huyo mwenye umri wa miaka 20 ambayo alipakia Instagram.

Masaa machache baadaye, Paul hata hivyo alidokeza kwamba hana mpango wa kuingia kwenye ndoa hivi karibuni.