"Ataniua!" Rayvanny alalamikia masharti magumu aliyopewa na mkewe baada ya kurudiana

Wawili hao walirudiana hivi majuzi baada ya kutengana miaka mitatu iliyopita.

Muhtasari

• Wawili hao walithibisha kufufuka kwa mahusiano yao yaliyosambaratika takriban miaka mitatu iliyopita, siku chache zilizopita.

• Rayvanny alieleza kuwa kufanya mazoezi ni mojawapo ya masharti ambayo mzazi mwenzake amemwekea baada ya kurudia.

Image: INSTAGRAM// RAYVANNY

Ni rasmi kwamba staa wa Bongo Raymond Mwakyusa almaarufu Rayvanny na mzazi mwenzake Fahymah wamerudiana.

Wawili hao walithibisha kufufuka kwa mahusiano yao yaliyosambaratika takriban miaka mitatu iliyopita, siku chache zilizopita baada ya Rayvanny kumshirikisha mpenziwe huyo katika video ya wimbo wake mpya 'Forever.'

“Mtoto mbichi teketeke aki Mama umelainika. Umeumbika, acha nikumwagie sifa. Waruke sakara na mateke uzuri wako hawatofika, mama umejazisha, mikate ya kumiminisha,” Rayvanny alimsfia Fahyma kwenye wimbo huo.

Takriban siku mbili baada ya kuachia wimbo huo, bosi huyo wa Next Level Music amethibitisha kuwa sasa hata wanaishi pamoja.

Kwenye ukurasa wake wa Instagram, alichapisha video yake na Fahyma wakiwa wametulia pamoja kitandani.

"Amka, amka.. Hongera, umetimiza milioni moja kwa siku moja," Rayvanny alisikika akimwambia mpenziwe Jumatatu.

Kwenye video nyingine aliyochapisha, msanii huyo wa zamani wa WCB alionekana nje akifanya mazoezi pekee yake.

Alieleza kuwa kufanya mazoezi ni mojawapo ya masharti ambayo mzazi mwenzake amemwekea baada ya kurudia.

"Haya ni masharti mapya ya shemeji yenu. Lazima nifanye mazoezi kila siku. Mimi nitakufa. Tuende," alisema kwenye video hiyo.

Mwimbaji huyo pia alimwonyesha mwanawe na Fahyma, Jaydan, akicheza na kuimba maneno ya wimbo wake mpya.

"Kashika ngome zoote," alisema.

Rayvanny na Fahymah walitengana mwaka wa 2019 ambapo kila mmoja aliamua kuenda njia yake. Baada ya kutengana, haikumchukua Rayvanny muda  mrefu kabla ya kuzama kwenye huba zito na bintiye Kajala, Paula Paul.

Hata hivyo, mwaka jana, bosi huyo wa Next Level Music alidokeza kuvunjika kwa mahusiano yake na mwanamitindo huyo wakati akitumbuiza katika tamasha la Fiesta 2022 mjini Sumbawanga, Tanzania.

"Mapenzi yasikuchanganye nakwambia, usije ukapata bila kama Dulla. Mapenzi usije kufananisha,  kama  vile chakula. Nilinyosha moyo Karula, nikaachana na Paula..." aliimba.

Mapema mwaka huu alidokeza kujuta kuvunjika kwa mahusiano hayo, na baadaye kidogo akadokeza kurudiana naye.

Mwezi Februari, Rayvanny alichapisha picha ya binti huyo wa muigizaji  Frida Kajala Masanja na chini yake kuambatanisha na emoji za moyo wenye moto, ambazo kwa kawaida hutumika kuashiria mapenzi.

"❤️‍🔥❤️‍🔥❤️‍🔥❤️‍🔥,"  aliandika kwenye picha nzuri ya kipusa huyo mwenye umri wa miaka 20 ambayo alipakia Instagram.

Masaa machache baadaye, Paul hata hivyo alidokeza kwamba hana mpango wa kuingia kwenye ndoa hivi karibuni.

Katika chapisho la Tiktok, mwanamitindo huyo aliiga sauti ya mwanamke akiweka wazi kuwa hayuko tayari kuolewa.

"Mwanaume akisema anataka kukuoa sasa hivi utamchukulia aje?" sauti ya mwanaume iliuliza kwenye video.

Sauti ya mwanamke ilijibu huku ilisema kwamba mtu ambaye ana nia ya kumuoa sasa anataka tu kumharibia maisha yake.

"Sitamchukulia vibaya. Si namkatalia tu. Anayetaka kunioa, anataka kuniharibia maisha,"