Zuchu aitikia wito wa Harmonize wa kununua Range Rover

Zuchu alionekana akipiga misele na gari hilo kwenye mitaa akiwa na ndugu zake na mama yake katika kiti cha mbele kando na dereva.

Muhtasari

• Zuchu anadai kununua Range Rover siku mbili tu baada ya Nandy kumnunulia mpenzi wake Billnass gari la Range Rover.

• Wasanii kuhaha kumiliki Range Rover ni baada ya Harmonize kudai kuwa kipimo cha msanii kamili ni kumliki Range Rover.

Zuchu anunua range rover.
Zuchu anunua range rover.
Image: Zuchu//Snapchat

Wiki moja baada ya Harmonize kuwachana wasanii wasiomiliki magari aina ya Range Rover, wasanii mbalimbali wa Kibongo sasa wameamua kuitikia wito wake na kutimba sokoni huku wakichomoa Range Rover nzito nzito.

Msanii Zuchu ni wa hivi punde kudai kujinunulia gari aina ya Range na kupiga misele nalo kwenye mitaa akiwa na familia yake ndani.

Zuchu ambaye amekuwa mvivu katika siku za hivi karibuni kupakia matukio kwenye Instagram yake, safari hii alipakia video hiyo kwenye ukurasa wake wa Snapchat.

Alionekana ndani akiwa na ndugu zake na mama yake wakizungumza mitaa ya jiji la Dar es Salaam huku wakiwa na furaha riboribo.

“Mdoli wangu mpya!” Zuchu aliandika kwenye video hiyo ya Snapchat.

Siku mbili zilizopita Radio Jambo iliripoti kuwa msanii Nandy alimnunulia mpenzi wake Billnass gari hio hilo aina ya Range Rover kama zawadi ya siku yake ya kuzaliwa.

Hii ni baada ya Harmonize kusema kuwa msanii yeyote ambaye hana gari la Range Rover basi hafai kujumuishwa kwenye orodha ya wasanii ambao wana uhakika na maisha yao ya Sanaa.

Wabongo wengine ambao hivi majuzi wamemiliki magari aina ya Range Rover ni pamoja na mdaku Juma Lokole, dadake Diamond Platnumz Esma Platnumz, Sishkiki Sikamatiki, mrembo aliyedaiwa kuwa mrembo wa Harmonize na wengine wengi.

Hata hivyo, watu wengi wanahisi kwamba wasanii wengi wanaoonesha magari hayo mitandaoni si yao katika maisha ya uhalisia.

Watu wanahisi kwamba ni aina mpya ya kiki ambayo imekuja ambapo kila msanii anaenda ‘showroom’ ya kununua magari na kukodisha gari hilo ili kupiga misele nalo kuwatishia watu na kuwaaminisha mashabiki wake mitandaoni kuwa yuko vizuri kimaisha.

Lokole Alhamisi alidai kuwa gari la Nandy kwa Billnass si la kweli kwa kile alisema kuwa aliomba kuoneshwa kadi ya umiliki wa gari lile lakini hakuoneshwa, na hivyo kutilia shaka kuwa gari hilo lipo chini ya miliki ya familia ya Billnass na Nandy.