Wiki baada ya Harmonize kuwakejeli wasanii wasio na Range Rover, Nandy amtoa aibu Billnass

Nandy alimpa mumewe Billnass Range Rover jipya kama zawadi ya kusherehekea siku yake ya kuzaliwa, Billnass alisema hajawahi miliki gari kama hilo.

Muhtasari

• Billnass alikuwa anasherehekea siku yake ya kuzaliwa Jumanne na mkewe Nandy alikuwa katika mstari wa mbele kabisa kumfanikishia siku hiyo.

• Billnass alisema kuwa gari kama hilo hajawahi kulimiliki hapo nyuma na kumshukuru sana mke wake.

Nandy amzawadi mumewe Billnass gari la Range Rover.
Nandy amzawadi mumewe Billnass gari la Range Rover.
Image: InstaGRAM

Msanii wa kike wa Bongo Fleva kutoka Tanzania Nandy amemfanyia mumewe Billnass jambo kubwa sana katika kusherehekea siku yake ya kuzaliwa Jumanne, kwa kumpa zawadi ya gari jipya aina ya Range Rover.

Katika video hiyo inayoonesha tukio zima, Billnass alifungwa macho kwa kitambaa na kuongozwa mpaka pale ambapo gari hilo lilikuwa limeegeshwa na kufunguliwa macho. Alikutana na bonge la surprise ambapo mbele yake aliona gari la Range Rover lenye rangi ya kijivu liiwa limezunguzwa utepe wa maua ya rangi ya maroon.

Kwa furaha isiyo mithilika, Billnass alimrukia mkewe Nandy na kumpa kumbato kama njia moja ya kuonesha shukrani kwa zawadi hiyo ambayo hakuwa ameitarajia.

Nandy alimwandikia ujumbe mtamu Billnass akimhakikishia upendo wake usio na mwisho huku pia akimhakikishia kuwa siku zote atashirikiana na yeye kufukuza madili ya pesa.

Nakupenda ️ @billnass no mara waaaaaa mshkaji wangu acha tufukuzie madili ya pesa 💸💸💸” Nandy aliandika.

Billnass alisema kuwa gari aina ya Range ni moja ya magari ambayo kwa muda mrefu amekuwa akitamani kumiliki.

"Ahsante mke wangu kwa zawadi kubwa sana, ni gari ambalo pia nimekuwa nikitamani na nimeendelea kutamani kuwa nalo. ni gari kubwa kwangu mimi kwa sababu sio ari amblo nimewahi kulimiliki hapo nyuma, kwa hiyo nashukuru sana," Billnass alisema.

Zawadi ya Nandy kwa mumewe inakuja siku chache tu baada ya msanii Harmonize kuibua makubwa akidai kwamba msanii yeyote kutoka ukanda wa Afrika Mashariki ambaye bado hajamiliki gari aina ya Range Rover hafai kumuongelesha hata kidogo.

Kulingana na Harmonize, gari aina ya Range Rover ndio mtindo mpya kwa wasanii wote na ndicho kigezo cha kuonesha kwamba msanii ana mafanikio kimuziki, huku kwake akilitaja gari hilo kama jambo dogo na pendwa kwake – alilifananisha kama mpenzi wake.

Ikumbukwe mwaka jana wakati alikuwa anahaha kushoto kulia kumbembeleza Kajala kumrudia, Harmonize alimnunulia Kajala gari aina ya Range Rover – Kajala 1- gari ambalo hata hivyo ilisemekana baada ya kuachana, Kajala aligoma nalo.