Zuchu amwagiwa mahaba na Diamond wiki chache baada ya kutangaza kuwa amechoka

Baadhi ya picha alizochapisha malkia huyo zilionyesha hisia za kimahaba kati yake na Diamond.

Muhtasari

•Zuchu alichapisha picha nzuri zikimuonyesha yeye na Diamond wakiburudika Dubai huku wote wakiwa wamevalia nguo nyeupe.

•Pia alishiriki video nyingine yao na wenzao wengine wakiburudika katika nchi hiyo ya jangwa.

Image: INSTAGRAM// ZUCHU

Mastaa wa Bongo Diamond Platnumz na Zuhura Othman almaarufu Zuchu wameendelea kuwachanganya mashabiki wao kuhusu hali halisi ya uhusiano wao.

Wiki chache tu baada ya wawili hao kudaiwa kutengana kufuatia tukio lililotokea wakati wa shoo ya Diamond, wanamuziki hao sasa wameonekana wakijivinjari jijini Dubai.

Siku ya Jumatano, Zuchu alichapisha picha kadhaa nzuri zikimuonyesha yeye na bosi huyo wa WCB wakiburudika katika nchi hiyo ya Mashariki ya Kati huku wote wakiwa wamevalia nguo nyeupe.

“DZ+DUBAI=DZUBAI,” Zuchu aliandika chini ya picha alizoweka kwenye Instagram.

Pia alishiriki video nyingine yao na wenzao wengine wakiburudika katika nchi hiyo ya jangwa.

Baadhi ya picha alizochapisha binti huyo wa malkia wa Taarab Khadija Kopa zilionyesha hisia za kimahaba, pengine kuashiria kuwa bado ni wapenzi.

Haya yanajiri wiki chache tu baada ya malkia huyo wa bongofleva kutoka Zanzibar kuandika taarifa kutangaza kuachana na bosi huyo wake katika WCB.

Katika taarifa yake mapema mwezi huu, mwimbaji huyo wa kibao 'Sukari' alieleza kuwa mpenzi wake Diamond amemfanya ashambuliwe kwa urahisi kupitia maisha yake yenye utata. Alimshutumu mpenzi huyo wake kwa kumweka kwenye hatari ya kutoheshimiwa na watu, jambo ambalo sasa amechoka nalo.

“I know mimi ni maarufu na kuongelewa ni kawaida. But kindly msipitilze kunipa sifa za uongo mradi kumpamba boss haswa kwa media ya nyumbani ambayo mnaweza pia kupata ukweli wa mambo mkasawazisha stori zenu,” Zuchu alilalamika kwenye ukurasa wake wa Instagram.  

Aliendelea, “Hii ndio sababu hasa kwa nini niliondoka, unachoka kuwa na mwanaume anayekusukuma kwa watu utukanwe na yeye ndo anayetumika kwenye kudhalilika kwako. Mwanamke wake ndo kanyagio la kila aliyemzunguka , akiamua tu basi yeye huungana nao na kuwapa vichwa vya kunivunjishia heshima ilhali umekaa kimya na unachofanya tu ni kukaa na kumeza. Ninajaribu kuwa mtu mzuri na kiungo dhaifu katika maisha yangu ni yeye."

Mwimbaji huyo mrembo alitoa wito kwa watu kuwa rahisi kwake na kumruhusu kuwa na amani.

Alilalamika kwamba kila jambo linapotokea linalohusisha watu katika maisha ya Diamond wakiwemo wazazi wenzake na wapenzi wake wa zamani, kila mara lengo linaelekezwa kwake.

“Hamkai kusema sababu yeye, anayesababisha mtu unataka kuondoka zake. Baby mama wakiamka na hasira waje na wao wanakutupia attitude zao kwa Zuchu. Maex nisiowajua content yao wanapewa wakusema ni Zuchu. Maadui zangu ashirikiane nao wakikaa na huyo mwanaume anawapa nguvu ni Zuchu,” aliandika.

Hapo awali, kulikuwa na tetesi kuwa aliondoka baada ya bosi huyo wa WCB kumtambulisha ex wake Sarah jukwaani wakati wa tamasha lililofanyika hivi majuzi nchini Tanzania.