"Nilikuwa karibu kupoteza maisha!" Size 8 akumbuka kipindi cha kutisha alipopoteza ujauzito

Tayari alikuwa amebeba ujauzito huo kwa miezi mitano wakati ambapo aliupoteza mnamo Oktoba 2, 2021.

Muhtasari

•Size 8 amekumbuka kipindi ambacho alipoteza ujauzito wa ambaye angekuwa mtoto wake wa tatu, takriban mwaka mmoja unusu iliyopita.

•Aliweka wazi kuwa tukio hilo ni moja tu ya sababu nyingi zinazomfanya sasa amtumikie Bwana kama mchungaji.

Image: INSTAGRAM// SIZE 8

Mwimbaji mashuhuri wa nyimbo za injili Linet Munyali almaarufu Size 8 amekumbuka kipindi ambacho alipoteza ujauzito wa ambaye angekuwa mtoto wake wa tatu, takriban mwaka mmoja unusu iliyopita.

Size 8 tayari alikuwa amebeba ujauzito wake kwa miezi mitano wakati ambapo aliupoteza mnamo Oktoba 2,  2021.

Akizungumza kupitia ukurasa wake wa Instagram siku ya Jumamosi, mama huyo wa watoto wawili alifichua kwamba wakati huo alikuwa amepoteza matumaini kabisa ya kuwahi kuwa mjamzito tena. Alisema alikuwa karibu kupoteza maisha pia kwani shinikizo la damu lilikuwa limemshambulia vibaya.

"Nikikumbuka siku hii, tarehe 2 Oktoba 2021. Nilikuwa nimetoka tu kupoteza ujauzito wa miezi 5, pia nilipoteza matumaini kabisa ya kupata ujauzito wowote katika siku za usoni na nilikuwa nikipigania maisha yangu, karibu nipoteze maisha yangu kutokana na shinikizo la damu kupindukia," alisema na kuambatanisha ujumbe huo na picha ya kumbukumbu iliyomuonyesha akiwa amelazwa hospitalini.

Mhubiri huyo alisema ni kwa neema ya Mungu kuwa alinusurika kusimulia na hiyo akamshukuru kwa kuokoa maisha yake.

Aliweka wazi kuwa tukio hilo ni moja tu ya sababu nyingi zinazomfanya sasa amtumikie Bwana kama mchungaji.

"Woi Baba yangu wa Mbinguni nakushukuru kwa kuhifadhi maisha yangu. Nisaidie kutumia zawadi hii ya uhai ulionipa kwa utukufu wako," alisema.

Mwaka wa 2021, mwanamuziki huyo alipoteza ujauzito wa ambaye angekuwa mtoto wao wa tatu kutokana na shinikizo la damu.

Katika mazungumzo ya mwaka jana, alifichua kwamba amekuwa akipambana na shinikizo la damu zaidi ya miaka mitano iliyopita.

Ugonjwa wa Size 8 ulitambulika baada yake kuzirai mtaani alipokuwa anaelekea nyumbani baada ya kutumbuiza katika tamasha ambayo alikuwa amehudhuria pamoja na mume wake, DJ Moh.

"Nilizirai nikiwa mjini nikapelekwa katika hospitali moja iliyokuwa pale. Hapo ndipo nikaambiwa shinikizo la damu yangu ni kubwa mno. Nilikuwa siko sawa. Kutoka siku hiyo nilianza kuchukua dawa za shinikizo la damu," alisimulia kupitia YouTube channel ya 'The Murayas'

Alisema ugonjwa huo ulikuwa ukimzidia mara kwa mara na kumfanya alazwe hospitali mara kadhaa tangu ulipogunduliwa.

Alisema amekuwa akipambana nao kwa ujasiri. Hata hivyo alikiri kwamba hivi majuzi ugonjwa huo ulikuwa umemwathiri kiasi cha kupatwa na msongo wa mawazo na kutaka kukata matumaini ya maisha.

"Mara hii haikuwa rahisi kwangu. Nilihisi nilikuwa nazama kwenye msongi wa mawazo.Kama sio neema ya Mungu nadhani ningekufa moyo kabisa.. Nilihisi kama kwamba nimechoka kupambana, nimechoka kuendelea, nimechoka kusubiri, nimechoka kusubiri muujiza. Mara nyingi sikuwa nahisi vizuri. Kuna wakati Moh alikuja katika chumba cha malazi na nikamwambia sihisi poa na nahisi kukata tamaa. Hiyo ni baada ya kutoka hospitali. Tulishiriki naye mazungumzo marefu," Alisema.

Size 8 alibainisha kwamba mume wake amekuwa guzo muhimu katika mapambano yake na shinikizo la damu. Alisema Mo amekuwa akimtia moyo na kumsihi asikate tamaa.