Unawezaje kutambua ikiwa dhehebu lako ni la itikadi potovu? Pastor T Mwangi aeleza

T Mwangi alisema ukiona mchungaji anakuuzia woga kuhusu matukio fulani basi hapo uko katika mafunzo ya itikadi kali na potovu.

Muhtasari

• "Kumbuka hakuna mwanadamu aliye juu ya Mungu na hakuna mwanadamu aliye juu ya viwango vya maandiko,” Mwangi alisema.

T Mwangi azungumzia dalili za kutambua kama kanisa lako ni la itikadi potovu.
T Mwangi azungumzia dalili za kutambua kama kanisa lako ni la itikadi potovu.
Image: Facebook

Mchungaji T Mwangi amefunguka kwa mapana jinsi ambavyo mtu unaweza kutambua iwapo kanisa ambalo unashiriki ibada ni la itikadi kali na za kupotosha.

Mwangi anatoa ufafanuzi huu wakati ambapo viongozi wa Makanisa wamewekwa chini ya shinikizo kutoa tamko lao kuhusu vifo vya waumini wa kanisa la mchungaji Paul Mackenzie huko Shakaola kaunti ya Kilifi.

Mpaka kufikia adhuhuri ya Jumatatu, polisi walikuwa wamefukua watu 67 kutoka shamba la ekari 800 la mchungaji huyo, shamba ambalo serikali ilitangaza kuwa makaburi ya jumla na vifo hivyo kuwa ni mauaji ya kimbari.

Mackenzie anadaiwa kuwashawishi waumini wa dhehebu lake la Good News International kujinyima chakula na maji kama njia moja ya kukutana na Mungu.

Kulingana na Mwangi, mchungaji wa kanisa la Life Church International huko Limuru, kuna dalili nyingi za kukufungua macho kutambua iwapo uko ndani ya dhehebu la itikadi potovu.

“Hapa ndipo unakuwa na kiongozi mmoja wa kiroho karibu katika kiwango cha kuwa Mungu. Anachukuliwa kama mungu wa dami. Maneno yake ni ya mwisho na hakuna anayeweza kuhoji maneno au matendo yake. Mtu huyo anaweza kuwa anafanya kazi chini ya karama fulani za mvuto hivyo basi kuidhinishwa. Wengine huajiri washiriki wao kupitia mafundisho ya kupindukia ya fundisho la heshima. Kumbuka hakuna mwanadamu aliye juu ya Mungu na hakuna mwanadamu aliye juu ya viwango vya maandiko,” Mwangi alisema.

Pia alisema kuwa ukiona mchungaji wa kanisa lako anajaribu kukejeli kila kanisa na kila mchungaji mwingine ili abakie kuwa yeye tu ndiye mchungaji halali basi hapo uko katika dhehebu lenye itikadi kali na potovu.

“Ubinafsi wa kila kitu, shule, vyombo vya habari, familia, jamii. Hiki ndicho kichocheo cha upotoshaji. Madhehebu mengi yanastawi kwa dhana hii. Baadhi ya watu wako katika madhehebu lakini wanafikiri wako katika harakati za kiroho,” Mwangi alisema.

Wengine watadai kuwa wamekutana na Yesu, Malaika au wazee wa zamani. Wanaishia kutoa nukuu za ziada za kibiblia na kufundisha kile ambacho hakiwezi kuthibitishwa kimaandiko. Hili ni eneo geni na wengi huishia kufundisha mafundisho ya ajabu, Mwangi alisema pia hii ni dalili ya kutambua upotoshaji.

Kando na hayo, wachungaji wengine pia utawapata wanakuuzia woga kwa kutumia matukio ya ajabu ambayo yanatokea, jambo ambalo Mwangi alisema ni ishara nyingine.