Maiti 20 zaidi yafukuliwa kwa shamba la pasta Mackenzie na kufikisha idadi kuwa 67

Kufikia Jumapili jioni, maiti 47 ilikuwa imefukuliwa kutoka kwenye makaburi hayo.

Muhtasari

• Utepe wa usalama umezungushwa kwenye shamba hilo ambalo limetajwa kuwa makaburi ya jumla.

• Polisi walitaja maafa hayo kuwa mauaji ya kimbari.

Baadhi ya miili ambayo ilitolewa Aprili 21, 2023.
Baadhi ya miili ambayo ilitolewa Aprili 21, 2023.
Image: ALPHONSE GARI

Jumatatu asubuhi maafisa wa idara ya DCI waliendeleza msururu wa kufukua maiti ya watu wanaodhaniwa kuwa waumini wa kanisa lenye maadili potovu la Good News International huko Shakahola kaunti ya Kilifi. Kanisa ambalo linaongozwa na mchungaji mwenye itikadi kali Paul Mackenzie.

Inspekta Jenerali wa polisi Japhet Koome ambaye alifanya ziara hiyo alisema kuwa miili 20 zaidi ilifukuliwa Jumatatu asubuhi na kufanya idadi hiyo kuongezeka hadi 67 kutoka 47 mnamo Jumapili jioni.

Wakati huo huo, watu 29 walikuwa wameokolewa wakiwa hai wakati polisi wakipitia eneo la Shakahola ambalo limezingirwa kufuatia operesheni hiyo.

Kiongozi wa ibada hiyo, Mchungaji Paul Makenzie Nthenge wa Kanisa la Good News International Church, anadaiwa kuwaagiza waumini kujinyima njaa ili "kukutana na Yesu."

Alishtakiwa mwezi uliopita baada ya watoto wawili kufa kwa njaa wakiwa chini ya uangalizi wa wazazi wao na yuko kizuizini.

Kufikia sasa, polisi wanasema wamewakamata waumini kumi na wanne wa ibada hiyo.

Mapema rais Ruto alimtaja Mackenzie kama kiongozi katili na jambazi sugu ambaye anatumia joho la utakatifu kueneza itikadi kali ambazo ni kinyume cha katiba.

Mackenzi amekuwa akishtumiwa kwa mafunz ya utata kwa waumini wake tangu mwaka 2015 ambapo alisemekana kuwaonya watoto dhidi ya kutafuta huduma ya elimu shuleni, watu kwenda hospitalini kwa huduma ya matibabu pamoja pia na kujinyima chakula na maji kama njia moja ya kukutana na Mungu moja kwa moja.

Shughuli ya kufukua maiti inaendelea katika shamba pana la ekari 800 la mchungaji huyo huko Shakahola kaunti ya Kilifi na tayari makaburi kadhaa yametambuliwa, huku yale ambayo yamefukuliwa yakipatikana kurundikwa na miili ya watu Zaidi ya wawili kwa pamoja.