Diamond amshauri Harmonize nini cha kufanya ili lebo yake ya Konde Gang ifaulu kama Wasafi

Lebo ya Harmonize iliporomoka pale ambapo Cheed, killy na Anjella waliondoka kwa kufuatana, Harmonize akisalia na Ibraah pekee.

Muhtasari

• Diamond alihisi Harmonize anajaribu kufunika nyota ya wasanii wake kwa kutowapa nafasi ya kuachia miziki yao.

• Alimshauri kwamba inafaa aache kutoa miziki ili kuwapa wasanii wake hiyo nafasi na kuwapa sapoti kwa kuisukuma mitandaoni.

Diamond na Harmonize
Diamond na Harmonize
Image: Screengrabs: YouTube

Diamond Platnumz bila shaka ndiye msanii wa pekee ambaye alikuja na wazo la kuanzisha lebo ya kuwasaini wasanii katika kipindi cha dijitali na kufaulu pakubwa.

Lebo yake ya WCB Wasafi ambayo haina miaka mingi kwenye tasnia ya muziki lakini tayari imewatoa wasanii wenye mafanikio makubwa ni moja kati ya lebo kubwa kwenye ukanda wa Afrika Mashariki.

Katika kipindi cha moja kwa moja mtandaoni na jamaa mmoja kutoka Ujerumani Diamond alifichua siri ambayo imeifanya Wasafi kusalia kidedea na kuwa na mafanikio makubwa, tofauti na lebo nyingine ambazo zimekuja nyuma na kudumaa ghafla.

“Kitu kimoja ambacho ninaweza washauri ni kwamba unahitaji kujitolea pakubwa kwa sababu kuwaongoza wasanii si kitu rahisi. Ndio maana unaona wasanii wengine wanaanzisha lebo na baadae unagundua lebo ile haipati mafanikio ya kufurahisha,” Diamond alisema.

Diamond alitoa ushauri kwa wasanii wenzake ambao wana wazo na kujaribu mkono wao katika kuanzisha lebo, huku ushauri wake ukimlenga aliyekuwa msanii wake Harmonize ambaye lebo yake ya Konde Music Worldwide ilianza kwa kasi lakini ikafika kipindi ikabuma na hata wasanii wengi kuondoka.

“Kama msanii unafaa kujitoa kwa asilimia mia. Wakati mwingine utahitajika kuacha kufanya muziki wako, kuacha kutoa muziki wako ili kuwapa wasanii wako nafasi ya kuachia miziki yao. Na hili wakati mwingine huwa gumu kwa baadhi ya wasanii kwa sababu bado wanataka wazidi kutamba.”

“Mimi nashauri kwamba hata kama utaacha kutoa muziki na uwape wasanii wake hiyo nafasi ya kutamba, hilo bado litakupa mafanikio kwa njia sawa,” Diamond alimshauri Harmonize japo hakumtaja moja kwa moja.

Baada ya kuondoka Wasafi, Harmonize alianzisha lebo yake ya Konde Music Worldwide ambayo ilishika moto kwa kasi na kuwapata wasanii wanne akiwemo Killy, Cheed, Ibraah na mwanadada Anjella.

Hata hivyo, misukosuko ilianza mwaka jana pale ambapo Cheed na Killy walivunja mikataba yao na wiki chache baadae Anjella akawafuata.

Harmonize sasa anasalia na msanii Ibraah pekee ambaye pia hasikiki kama alivyokuwa akisikika mwanzoni, kwani Harmonize hata siku hizi hamzungumzii achia mbali kutangaza muziki wake.