Bien msanii wa 4 wa Kenya baada ya Akothee na Tanasha kufanya collabo na Diamond

Kando na Akothee na Tanasha Donna, Diamond pia aliwahi fanya collabo na msanii Victoria Kimani.

Muhtasari

• Alisema kuzingatia urafiki huo wa muda mrefu, wamehisi ni muda sasa kuingia studioni na kuwabariki mashabiki wao na kibao cha moto.

Bien Baraza adokeza collabo na Diamond Platnumz.
Bien Baraza adokeza collabo na Diamond Platnumz.
Image: Instagram, Maktaba

Kiongozi wa bendi ya Sauti Sol, Bien Baraza amefichua kwamba kuna collabo ambayo iitatoka hivi karibuni wakiwa na msanii namba moja wa muda wote kwa miziki ya Bongo Fleva, Diamond Platnumz.

Katika mazungumzo na SPM Buzz, Baraza alionesha jinsi gani anamkubali Platnumz na hata kujifunza kutoka kwake masuala mengi sit u muziki bali pia katika sekta ya ujasiriamali.

Bien alisema kuwa kwa muda mrefu wamekuwa marafiki na Platnumz na hata kipindi cha kuchipukia kwenye tasnia hiyo yenye ushindani Zaidi ya miaka 10 iliyopita walianza pamoja.

Alisema kuzingatia urafiki huo wa muda mrefu, wamehisi ni muda sasa kuingia studioni na kuwabariki mashabiki wao na kibao cha moto.

“Kusema ukweli tu Diamond ni mtu wangu wa karibu, tumekuwa marafiki kwa miaka mingi Zaidi kitambo kile tukianza kama chipukizi. Yule bwana ni rafiki wangu na ni heshima kubwa kwa msanii mwenye uzoefu mkubwa kama yeye kukubali muziki wangu, lakini pia mimi naukubali sana muziki wake,” Bien alisema.

“Ni mtu wa ajabu sana na ananihimiza kwa njia nyingi tu, kutoka kwa kuwa mjasiriamali, mienendo yake – ni msanii wa maana sana katika taifa hili, barani Afrika na hata kote ulimwenguni. Na collabo iko inakuja,” Bien aliongeza.

Msanii huyo alifuchua haya baada ya video ambayo haijulikani ni ya muda gani kuenezwa ikimuonesha Diamond akiimba kwa mbwembwe wimbo wa Bien – Inauma – huku akiendelea na shughuli zake ndani ya jumba moja la kifahari.

 Endapo collabo hiyo yao itafanikishwa, Bien atakuwa msanii wa nne katika historia ya Kenya kimuziki kufanya ngoma na Diamond Platnumz baada ya Akothee, Victoria Kimani na Tanasha Donna kufanya hivyo.

Kwa kuonesha urafiki wao wa muda mrefu kwa vitendo, mwaka mmoja uliopita baada ya Diamond kufanya makosa katika kuzungumza lugha ya Kiingereza kwenye sehemu ya kwanza ya filamu ya uhalisia ya Netflix, Young Famous & African, Bien aliwasuta vikali waliojaa mitandaoni kukejeli kiingereza cha Diamond akisema kwamba mafanikio si kuwa na weledi katika lugha ya Mkoloni.