Warembo mnaotingisha makalio TikTok mnajua kujiheshimu kweli? - Willy Paul auliza

Mnamo Februari mwaka huu, Pozee aliwashauri wanaume wanaotaka kuoa kuepuka kabisa mtego wa wasichana wa mijini 'waliojanjaruka' na badala yake kuwaendea vienyeji wa vijijini.

Muhtasari

• “Sio vibaya lakini kila muda kumbuka kwamba chenye unachomwonesha mwanaume ndicho atakachokujia kwako" - Pozee alisema.

• Mwezi Februari Pozee aliwataja wasichana wa Instagram na TikTok kama sumu na kuwatahadharisha wanaume dhidi ya kuchumbiana nao.

Willy Paul atoa neno kuhusu wasichana wa kutingisha maungo TikTok.
Willy Paul atoa neno kuhusu wasichana wa kutingisha maungo TikTok.
Image: Instagam

Msanii wa kizazi kipya wa Kenya Willy Paul amepeleka kwenye mitandao yake ya kijamii kuonesha kutoridhishwa kwake na tabia ya baadhi ya warembo ambao aghalabu hujianika kwenye mtandao wa TikTok wakionesha maungo na mapozi yao.

Pozee ambaye alionekana kutofurahishwa na hulka hiyo aliwapa ushauri uliokolezwa munyu warembo hao akisema kuwa kutingisha makalio yao bila stara mara nyingi kunaonesha kina cha kukosa kujiheshimu.

Msanii huyo alisema kuwa wengi wa warembo wanaofanya hivyo hukosa kujiheshimu huku wakitafuta umaarufu kutoka kwa wasanii ili waone na kuchukua video ile na kuichapisha kwenye mitandao yao pia.

“Kusema tu ukweli hawa wasichana wanaotingisha makalio TikTok ili wasanii waone na kuchapisha pia huwa wanakumbuka kuna kitu kinaitwa kujiheshimu kweli?” msanii huyo mkali wa kibao cha Umeme aliuliza.

Pozee alisema kuwa wasichana hao wasichokijua ni kwamba wanachokionesha kwa wasanii hao ndicho wanakujia kutafuta kwao na mwisho wa siku wao ndio hubaki wakijilaumu kwa maamuzi mabaya wakati tayari mwiba umeshawachoma.

“Sio vibaya lakini kila muda kumbuka kwamba chenye unachomwonesha mwanaume ndicho atakachokujia kwako, lakini pia kama hilp ndio lengo lenu basi hamna tatizo endeleeni kutingisha,” Willy Paul alitia kikomo.

Hii sio mara ya kwanza kwa mwimbaji huyo wa zamani wa Injili kushiriki maoni yake kwenye TikTok na wasichana wa Instagram.

Mnamo Februari mwaka huu, Willy Paul aliwashauri wanaume wenzake kujiepusha na wanawake wanaohangaishwa na mitandao ya kijamii.

Katika maelezo yake, wasichana wa Instagram na TikTok ni sumu na ni afadhali kupata mchumba kutoka kijijini kwa sababu wasichana ‘walijanjaruka’ hucheza michezo mingi na kufukuzia pesa tu.

“Jambo moja ambalo nimegundua kuhusu wasichana hawa wa Instagram ni kwamba wote ni sumu. Wanaume wenzangu tuwatafute wanawake wa maana huko vijijini, tuwafanye wang'ae tunavyotaka. Tiktok na Instagram ni pepo tu. Dakika hii uko naye, dakika chache zijazo utaona Mombasa na baba Kamau na amebadilisha jina,” Pozee alitema ushauri.