Willy Paul: Wanawake wa Insta na Tiktok ni sumu, wanaume tafuta vienyeji

"Wanaume wenzangu, hebu na tukatafute wanawake wa maana vijijini, tuwasafishe wang’are vile tunataka" - Pozee.

Muhtasari

• Msanii huyo alisema wanawake wa mitandaoni ni wajanja ambao hawatulii sehemu moja kama popo.

Image: INSTAGRAM// WILLY PAUL

Msanii wa kizazi kipya mwenye utata Willy Paul kwa mara nyingine ametoa ushauri wa wanaume kuhusu msichana wa kutoka kimapenzi naye siku chache kuelekea siku ya wapendanao ya Valentino.

Pozee alishauri kuwa kama wewe ni mtoto wa kiume na unahisi uko tayari kuingia kwenye kidimbwi cha mapenzi, basi kuna moja unafaa kufahamu kuhusu mwanadada anayekufaa.

Kulingana naye, wanadada wote ambao wana uraibu wa mitandao ya kijamii haswa Instagram wote hawafai kuwa katika darubini zako wewe kama mwanamume, kwani hao wanadada wengi wao ni sumu.

Alishauri kuwa msimu huu wa Valentino, kila mwanamume anayejipenda na kujiheshimu basi akatafute mwanadada wa kijijini.

“Kitu kimoja ambacho nimegundua kuhusu hawa wanadada wa Instagram wote ni sumu. Wanaume wenzangu, hebu na tukatafute wanawake wa maana vijijini, tuwasafishe wang’are vile tunataka. Hawa wa Tiktok na Instagram ni mapepo tu,” Willy Paul alishauri.

Alifafanua Zaidi kuhusu ushauri wake akisema kuwa wanadada wa Instagram si wa kutulia sehemu moja kwani wanahaha pande zote kama popo, dakika hii yuko nawe hapa dakika nyingine ndio yule amepaa unamsikia yuko Pwani.

“Dakika hii mko naye hapo, dakika chache zijazo unamuona Mombasa ako na baba Kamau na hadi amebadilisha jina,” Pozee alisema.

Ushauri wake kwa kiasi Fulani unawiana na ule wa msanii wa injili Daddy Owen ambaye mwishoni mwa mwaka jana aligonga vichwa vya habari akisema alikuwa anataka mwanamke wa kuoa.

Katika tangazo lake, Owen alisema kigezo kikubwa ni kwamba mwanamke huyo sharti awe wa kutoka kijijini yaani ‘kienyeji’ kwa lugha ya vichochoroni, akisema kwamba wanawake wa mijini wenye weledi wa kutumia kila mitandao mipya ya kijamii si wanawake wa kuolewa.