Rosa Ree: Mimba yangu ilikuwa inachukia harufu ya vitunguu na friji

Rosa Ree alisema kuwa kutokana na mtindo wa muziki ambao anaoimba [HipHop], alikuwa anajichukuliwa kuwa gaidi lakini mimba ilimnyoosha na kumnyenyekesha.

Muhtasari

• Rosa Ree alisema kuwa mimba yake ilimbadilisha uso kabisa kiasi kwamba viungo kama pua lilinenepa.

• Simu yake ambayo alikuwa ameweka ‘facial recognition’ ili kuifungua, haikuwa inamtambua kama ni yeye.

Rosa Ree amefunguka jinsi mimba yake ilivyompelekesha.
Rosa Ree amefunguka jinsi mimba yake ilivyompelekesha.
Image: Screengrab//SimuliziNaSauti

Rapa bora wa mwaka 2022 kwa mujibu wa tuzo za Tanzania Music Awards, Rosa Ree kwa mara ya kwanza amefunguka kwa uhakika kuhusu safari ya ujauzito wake, wiki chache baada ya kupakia picha za jinsi ujauzito ulivyombadilisha muonekano wake.

Katika mahojiano na blogu moja nchini mwao, Rosa Ree alisema kuwa safari yake ya ujauzito ilikuwa ya kufana na ya kukumbukwa licha ya kwamba ilikuja na changamoto zake lakini pia kulikuwepo na mazuri ambayo siku zote ataishi kuyakumbuka.

“Ni safari ambayo ni ndefu sana ambayo ni kutoka wakati niligundua nina mimba, namsubiria mwanangu hadi mwisho wa Dahari, unajua huachi kuwa mama. Imenibadilisha sana, imenifanya nijipende Zaidi na kujijua kwa kiwango tofauti kwamba kwa kweli mimi ni mkakamavu,” alisema rapa huyo.

Rosa Ree alisema kuwa kutokana na mtindo wa muziki ambao anaoimba [HipHop], alikuwa anajichukuliwa kuwa gaidi lakini mimba ilimnyoosha na kumnyenyekesha.

Kama wanawake wengine wajawazito, Rosa Ree pia alikuwa na matamanio ya baadhi ya vitu na kuna vingine ambavyo hakuwa anavitaka kabisa kumkaribia.

“Nilipenda chakula. Nilikuwa napenda sana kula. Nilikuwa naamka saa tisa asubuhi kupika lakini nilikuwa nachukia sana vitunguu. Harufu ya vitunguu sikuwa napenda kabisa. Yaani hata chakula kikipikwa na kitunguu heri nisikione. Halafu pia sikuwa napenda harufu ya friji,” msanii huyo alisema.

Rosa Ree alisema kuwa mimba yake ilimbadilisha uso kabisa kiasi kwamba viungo kama pua lilinenepa hadi simu yake ambayo alikuwa ameweka ‘facial recognition’ ili kuifungua, haikuwa inamtambua kama ni yeye.

“Wakati mwingine hata facial recognition kwenye simu ilikuwa inanikataa, tulikuwa watu wawili tofauti. Mimi mwenyewe nilijishangaa huyu ni nani, nilikuwa sijiangalii sana kwenye kioo kwa sababu nilikuwa simjui yule niliyekuwa naona. Lakini alituletea kitu kizuri duniani,” Rosa Ree alisema baina ya kicheko.

Rapa huyo alidhihirisha kwamba furaha yake yote ilichukua mkondo kwenda kwa mwanawe na kumtaja kuwa mpole ambaye kila asubuhi anaporauka kumuangalia tabasamu lake tu humpa faraja kuwa alifanya uamuzi mzuri wa kuwa mama.