Rosa Ree, msanii wa rap akiri kwa kilio kuwa hayuko sawa, "maisha yangu ni sinema!"

" Lakini leo nakiri kwamba SIKO SAWA! Napitia mambo mazito mpaka naona giza tu. " Rosa Ree alisema baina ya kilio cha uchungu.

Muhtasari

• "Nawaza wakati mwingine kuwa wazi na haya ninayoyapitia ila nashindwa maana najua wengine watanicheka" Rosa Ree alikiri.

• Msanii huyo alisema kwamba anapata wakati mgumu kuzungumza anachokipitia kwa sababu hawezi pata msaada zaidi ya kupigiwa simu ili kufanya mahojiano kwa media kupata maudhui.

Rosa Ree, msanii wa rap alia kwenye video akisema hayuko sawa.
Rosa Ree, msanii wa rap alia kwenye video akisema hayuko sawa.
Image: Insatgram

Msanii wa Rap kutoka nchini Tanzania Rosa Ree amevunja kimya chake kwa kilo cha uchungu akikiri kwamba hayuko sawa kisaikolojia n kiakili.

Kupitia video ambayo Ree aliipakia kwenye ukurasa wake wa Instagram, alisimulia kwa mapana na marefu jinsi amekuwa akipitia wakati mgumu lakini kulazimika kuficha huzuni wake nyuma ya tabasamu la kughushi ili kuwafurahisha mashabiki wake.

SIKO SAWA! Mara nyingi naulizwa “Uko aje?” Nasema “Niko sawa” kusema tu ila sio kumaanisha. Lakini leo nakiri kwamba SIKO SAWA! Napitia mambo mazito mpaka naona giza tu. Inaumiza kwamba haijalishi ninachopitia lazima niendelee kuonyesha furaha kwenye mitandao kana kwamba niko sawa. Kila siku napaswa niendelee kutimiza jukumu la kuwaburudisha, kupromote album, kutoa ngoma mpya, kurekodi, kushoot videos na kuhimiza jamii…” Rosa Ree alieleza kwa kilio.

Mkali huyo wa HipHop kwa wasanii wa kike alikiri waziwazi kwamba kuna mambo mazito anayoyapitia maishani mwake lakini hakuna mtu anayejua.

Alisema hajui mtu wa kumwendea kwa ajili ya msaada, licha ya kuwa na mashabiki wengi ambao wamepata burudani hadi kushiba kutoka kwake.

Msanii huyo alionesha kujuta kwamba hata angezungumza kinachomsibu basi asingepata msaada Zaidi ya kuwa gumzo kwenye blogu za udaku tu.

“Mmepata burudani kutoka kwangu ila nikiwa sipo sawa mnanisaidiaje?? Nawaza wakati mwingine kuwa wazi na haya ninayoyapitia ila nashindwa maana najua wengine watanicheka, wengine watanisema, wengine watanitenga na wengine hawatajali kabisa. Nyinyi si ndio familia yangu, sasa wapi niende?"

"Nikizungumza ninayoyapitia yatakuwa tu vichwa vya habari kwenye kurasa za udaku? Nitapigiwa simu kufanya mahojiano ili media zipate stori? Yaani maisha yangu ni sinema tu kwa ajili ya kuwapa watu views? Na hisia zangu je? Na hata nikiwa sipo maisha si yataendelea tu????…..Kusema ukweli SIKO SAWA!" Msanii huyo alilia.