Msanii wa injili ashinda kesi ya hakimiliki dhidi ya bendi aliyoianzisha kisha kufukuzwa

Kaki Mwihaki alianzisha bendi ya injili ya Adawnage mwaka wa 2008 lakini ilipofika mwaka 2015, mzozo ulianza baina yake na wanabendi wenzake.

Muhtasari

• Mwihaki ambaye baadae alihamia Marekani alianzisha mchakato wa kesi akitaka kupewa hakimiliki za nyimbo 12 kati ya 20 alizoshiriki kutunga katika albamu za kwanza 2.

• Kupitia kwa wakili wake, Mwihaki alidai kwamba hajakuwa akipokea mirahaba kwa zaidi ya miaka 6.

Kaki Mwihaki, mwanzilishi wa kundi la Adawnage.
Kaki Mwihaki, mwanzilishi wa kundi la Adawnage.
Image: Instagram

Mwanamuziki wa injili Roseline Kaki Mwihaka ameshinda kesi ya hakimiliki aliyowasilisha dhidi ya bendi yake ya Adawnage.

 Mzozo wa Mwihaki na bendi ya dawnage ulianza takribani miaka mitatu iliyopita baada ya kujiondoa kwenye kundi hilo na kuanza kutunga na kuimba nyimbo zake za injili kama msanii binafsi.

Bendi ya injili ya Adawnage ilianza mwaka 2008 iimjumuisha Mwihaki ambaye alikuwa mwanzilishi, David Ogara, Robert Njuguna, Anthony Akivembe na wengine.

Kwa muda wa miaka minane bendi hiyo ilitumbuiza kwa pamoja nchi nzima, ilipata sifa na kuzunguka dunia huku Mwihaki akiwa mwimbaji mkuu na mwanzilishi wake.

Baada ya kutamba na vibao vingi vilivyowabaribi wengi wa Wakenya, kundi hilo lilikumbwa na msukosuko uliopelekea mwanzilishi wake Mwihaki kuanzisha mchakato wa kesi akidai hakimiliki za miziki ya bendi hiyo.

Wiki iliyopita, Mwihaki, ambaye kwa sasa anaishi Arizona, Marekani, alishinda kesi ya hakimiliki dhidi ya Adawnage ambapo anataka kulipwa mirabaha yake kwa kipindi cha zaidi ya miaka sita. Anashutumu bendi hiyo kwa kukusanya pesa za mrabaha na kutomrudishia sehemu yake, jarida moja liliripoti.

Kulingana na wakili wake David Katee, Mwihaki, ambaye sasa anafahamika kwa jina Kaki Mwihaki, sasa atatafuta maagizo ya mahakama ili kushurutisha bendi hiyo kumfidia.

Kulingana na jarida hil, Mwihaki anatazamia kufidiwa mamilioni ya pesa kutokana na mirabaha ambayo bado hajakuwa akilipwa sit u kwa wimbo mmoja bali kwa nyimbo Zaidi ya 10.

Masaibu yake na bendi ya Adawnage yalianza mwaka wa 2015 wakati ndoa yake iliyumba na kutokana na mchakato mgumu wa talaka, alilazimika kujiondoa kama mwimbaji mkuu wa bendi huku akishughulikia talaka, ambayo ilimuathiri kisaikolojia na kiafya pia.

Ni kipindi hicho ambapo wanabendi wengine waliingia katika mikataba mbalimbali pasi na kumshirikisha Mwihaki ambaye alikuwa amedhoofishwa na ndoa yake kusambaratika.

Haikuchukua muda mrefu kabla ya kufukuzwa kwenye bendi yake na kunyimwa ufikiaji wa orodha ya muziki ya Adawnage. Baadaye Mwihaki alihamia Marekani. Akiwa Marekani, Mwihaki aliifikia bendi hiyo akiomba kulipwa mirabaha yake ya nyimbo 12 kati ya 20 zilizomo katika albamu mbili za mwanzo - Safari na Maisha - alizozitunga na kuziandika, jambo ambalo wanabendi walikataa na kuanzisha vita vya hatimiliki dhidi yao.