DJ Brownskin ana hatia ya kuacha watoto washuhudie mama yao akinywa sumu - Wakili Omari

Danstan Omari alisema chini ya sheria ya kuwalinda watoto, DJ Brownskin ana kosa kubwa kwani watoto wataathirika kisaikolojia kutokana na kitendo kile.

Muhtasari

• Wakili Omari alisema kwamba sheria ya kuwalinda watoto itamkaba DJ Brownskin kwa kuwaathiri kisaikolojia.

• Kuwaweka watoto waone mtu akijitoa uhai ni hatia kali chini ya sheria ya watoto - Omari alisema.

Wakili Omari amesema DJ Brownskin anaweza kushtakiwa chini ya sheria ya kuwalinda watoto.
Wakili Omari amesema DJ Brownskin anaweza kushtakiwa chini ya sheria ya kuwalinda watoto.
Image: Instagram, Facebook

Wakili Danstan Omari ametoa maoni yake kuhusu video inayoenezwa mitandaoni ikimuonesha DJ Brownskin akimrekodi mke wake akinywa sumu hadi kufa mbele ya watoto wake.

Kulingana na wakili huyo mjuzi wa sheria, DJ Brownskin anaweza kuchukuliwa hatua za kisheria kwa kufanya kitendo kile pasi na kuchua hatua yoyote kuzuia.

Omari alitofautiana na wakili mwenzake Cliff Ombeta aliyesema kwamba Brownskin hana makossa kwani hakuhusika katika kumkorogea mkewe sumu, na kitendo cha kurekodi video kilikuwa ni kupata ushahidi wa kujitetea kwamba hakuhusika katika kitendo cha mkewe.

Omari anasema kwamba katika sheria inayowalinda watoto, DJ Brownskin anaweza chukuliwa hatua kwa kusimama nao na kushuhudia kwa macho yao mtu akifanya jaribio la kujitoa uhai mbele yao.

“Kama unakosa kuzuia uharibifu kufanyika, hilo ni kosa kisheria. Kama utasimama na watoto mkiangalia mtu akijitoa uhai, hilo ni kosa kisheria chini ya sheria ya kuwalinda watoto. Hiyo ni kuwadhulumu watoto kisaikolojia kwa sababu watoto hao hawatakuja kusahau picha ile kichwani mwao,” Omari alisema.