Anjella aeleza kupitia video jinsi Kajala alichangia kuondoka kwake Konde Gang

Anjella alitumia Harmonize na Kajala wa kimchongo kwenye video hiyo kuonesha jinsi Kajala alivyokuwa anafanya maamuzi kwa niaba ya Harmonize kuhusu wasanii Konde Gang.

Muhtasari

•Katika scene moja, Harmonize na Kajala walionekana pamoja wakati Anjella aliingia kuomba hela kwa Harmonize.

• Harmonize anaingia mfukoni na kutoa hela lakini Kajala anamzima kabisa asimpe Anjella hela.

Anjella atumia Harmonize na Kajala wa mchongo kuonesha kilichomtoa Konde Gang.
Anjella atumia Harmonize na Kajala wa mchongo kuonesha kilichomtoa Konde Gang.
Image: Screengrab//Anjella.

Ikiwa ni miezi kadhaa baada ya msanii Anjella kujiondoa rasmi katika lebo ya Konde Gang, msanii huyo hivi majuzi amevunja ukimya wa mitandaoni kwa kuachia kibao chake kipya kabisa tangu kuondoka kwa Harmonize.

 Katika kibao hicho kipya kwa jina Blessing ambacho alikiachia wiki moja iliyopita, siku moja iliyopita pia ameachia video ambayo imekuwa gumzo kubwa mitandaoni.

Katika ngoma hiyo, Anjella ametumia fursa kubwa kusimulia maisha yake jinsi alivyopatana na Harmonize na kumshika mkono huku azma yake ikiwa ni kuyaondokea maisha ya mihangaiko.

Gumzo kubwa hata hivyo si simulizi yake, bali ni kile alichokionesha kuweka uzito na kiimbo Zaidi kwa kutumia picha za watu wenye mfanano wa aliyekuwa bosi wake Harmonize lakini pia mwanamke aliyekuwa na mfanano wa Kajala Masanja, ambaye mpaka kipindi Anjella anaondoka, alikuwa mpenzi wa Harmonize.

Bila kuzungumzia kile ambacho Anjella alikuwa akikisema katika matukio ambapo wawili hao walionekana kwenye ngoma, vitendo vyao vilionekana na kuashiria kwa kiasi kikubwa jinsi mwanamke huyo – Kajala kwa muktadha huu – alivyochangia pakubwa Anjella kuzimiwa ndoto yake Konde Gang.

Harmonize na Kajala – wote wa mchongo – wanaonekana kwenye scene moja wakiwa kitandani wametulia hivi wakati Anjella anaingia na kuonekana kuomba pesa kutoka kwa bosi wake Harmonize.

 Kweli Harmonize huyo kwenye video anazama mfukoni na kuchomoa noti kadhaa ambazo anamnyooshea Anjella kuchukua lakini hapo hapo Kajala anamshika Harmonize kwa haraka na kumkataza kwamba hakuna senti hata moja ambayo Anjella anafaa kupewa.

“Kuna muda mapenzi yanaweza kakutoa kweli reli, maana kuna wapenzi wanapenda kukuona unavyofeli. Na tatizo la mapenzi, mapenzi yana nguvu kweli kweli…” Anjella anaimba kwenye scene ya tukio hilo.

Wachanganuzi wa video hiyo walihisi kwamba hapa Anjella alikuwa anajaribu kujitoa makovu kwa kuweka wazi kilichosababisha yeye kuondoka Konde Gang, baada ya makundi ya watu kadhaa kuzungumza maoni na uvumi tofauti tofauti.

Kwa mujibu wa kitendo hicho, Kajala alimkomalia Harmonize kutowajali wasanii wake, huku hela zote akitaka zibaki kwake na hivyo kuifanya iwe vigumu kwa wasanii hao kutusua katika lebo hiyo – kilichosalia ni kujitoa tu.