Willis Raburu atangaza kuondoka kwenye runinga ya Citizen baada ya miaka 13

Mtangazaji huyo alitangaza uamuzi wake kuondoka na kusema haikuwa rahisi kwake.

Muhtasari

• Willis Raburu ametangaza kuondoka katika runinga hiyo baada ya kuhudumu kwa muda wa takriban miaka 13.

•Raburu aliwashukuru wafuasi wake ambao wamempa sapoti kwa miaka 13 ambayo amehudumu kama mwanahabari.

Willis Raburu katika studio za Radio Jambo
Image: RADIO JAMBO

Mtangazaji wa Citizen TV, Willis Raburu ametangaza kuondoka katika runinga hiyo baada ya kuhudumu kwa muda wa takriban miaka 13.

Katika video alizochapisha katika akaunti zake za mitandao ya kijamii, Willis alitangaza uamuzi wake kuondoka na kusema haikuwa rahisi kwake.

"Nimefanya uamuzi wa kuondoka Royal Media Services na imekuwa uamuzi mgumu sana kwangu."

Baba huyo wa mtoto mmoja alifichua kuwa aliweza kuwasilisha barua ya kujiuzulu mwanzoni mwa mwezi Juni na shirika hilo lilipokea habari hizo vyema na kuweza kumsaidia katika safari ya kuondoka.

"Tangu nilipowasilisha barua ya kujiuzulu mwanzoni mwa mwezi Juni mpaka sai wamekuwa watu wazuri kwangu katika mapito haya."

Raburu aliwashukuru wafuasi wake ambao wamempa sapoti kwa miaka 13 ambayo amehudumu kama mwanahabari, aliwashukuru pia wafanyi kazi wenzake.

"Nina shukrani kuu kwako shabiki kwa kutembea nami kwa miaka 13 ya safari ya uanahabari, ninawashukuru pia wafanyi kazi tuliofanya nao kazi kwa muda huu."

Nini kinafuata sasa , "Nitapumzika, nataka nipumue, nataka nishiriki maarifa niliyonayo na pia niendelee na masomo yangu ya uzamili katika chuo kikuu cha USIU."

Willis aliongeza kuwa ameweza kuandika kitabu kinachosimulia hadithi yake ya miaka mingi katika taaluma ya uanahabari. Aliwahimiza mashabiki wake kulinunua. Alifichua kuwa kitabu hicho kitaitwa 'Undefined'.

"Unajua nini? nimenakili kila kitu kilichofanyika ndani ya miaka 14 katika kitabu, ninakiita kutabu hicho 'Undefined' kwa sababu nimefanya vitu mingi."