Wema Sepetu atokwa na machozi kwa alichoandikiwa na watu kuhusu kukosa mtoto

Wema aliandikiwa jumbe nyingi baada ya kuonekana akimjali sana mtoto wa mpenziwe Whozu na ex wake Tunda wakati wa kusherehekea siku yake ya kuzaliwa kufikisha miaka miwili.

Muhtasari

• Wanamitandaoni waliona jambo hilo kuwa la heri na hawakusita kumwandikia Wema jumbe za kumfariji kwa kukosa mtoto kwa muda mrefu.

Wema Sepetu akiwa na mtoto wa Whozu na ex wake Tunda.
Wema Sepetu akiwa na mtoto wa Whozu na ex wake Tunda.
Image: Instagram

Mwigizaji Wema Sepetu ametokwa na machozi ya furaha na kuonesha shukrani na faraja yake kwa jumbe nyingi ambazo mashabiki wake walimuandikia kwenye chapisho la picha alizopakia akisherehekea siku ya kuzaliwa na bintiye mpenzi wake Whozu.

Lola, mtoto wa Whozu na Ex wake Tunda alikuwa anasherehekea kufikisha umri wa miaka 2 na Wema alisimama kama mama kwa mtoto huyo kusherehekea pamoja na Whozu.

Wanamitandaoni waliona jambo hilo kuwa la heri na hawakusita kumwandikia Wema jumbe za kumfariji kwa kukosa mtoto kwa muda mrefu, na kwa jinsi alivyoonesha mapenzi yake kwa mtoto huyo bila kumbagua kuwa si wake.

Wema akitoa shukrani zake kwa mashabiki waliomtumia jumbe za faraja, alizidiwa na hisia na kusema kuwa anawaza tu Mungu angezisikia dua zao na kumjibu ombi lake la kupata mtoto, kwani ana uchu sana kumpakata mwanawe siku moja pia.

Maombi yenu ni Mengi na Makubwa sana... 🥺🥺🥺 Mi naomba niseme tu Asante... Nawaza tu kwa mbali ndo Allah kaskia maombi yenu na kutenda jambo.... 🤗🤗🤗Uwiiiiii.... Aaaah mi sijui bhaaanaaa....Lakini mbali na yote, Moyo wangu umejawa na Furaha nyingi sana…” Wema aliandika.

Wema alisema kuwa kuna muda mwingine anawaza kuchoka na kutamauka lakini anapoangalia nguvu na jumbe chanya kutoka kwa watu Zaidi ya milioni 10 wanaomfuatilia Instagram, basi anapata furaha na sababu ya kujikung’uta mavumbi na kuendelea kujitia moyo hata Zaidi kwamba ipo siku naye atabarikiwa na mwanawe.

“Sina lolote maskini ya Mungu ila nina furaha mwenzenu.... 💞💞💞. Unaweza kosa vingi ila Mungu akaamua tu kukufariji kwa namna yake... Faraja hio ninayo Alhamdulillah... Mungu nitunzie hii faraja yangu... 😍 Ibakie tu 🥺” aliandika.

Katika mahojiano na Haji Manara miezi michache iliyopita, Wema alisema kuwa bado hajachoka kupambana kupata mtoto wake, licha ya kudanganywa na kuhadaiwa na wengi kuhusu dawa za kiasili ambazo hata hivyo hazijafua dafu kwa upande wake.

Hata hivyo, mwigizaji huyo mkongwe pia aliashiria kwamba huenda tumbo lake lina matatizo kwa kile alidokeza kwamba ni uavyaji mimba ‘mara kidogo’ lakini akafutilia mbali kuwa hiyo ndio inaweza kuwa sababu ya kukosa kushika mimba akisema kuwa ‘ninawajua wengi walioavya mimba nyingi na baadae wakapata watoto’.