Siwezi sahau kitu ambacho Diamond alinifanyia miaka zaidi ya 10 iliyopita - MP Jalang'o

"Diamond mara ya kwanza kukutana, tulikuwa tumeitiwa shoo Malindi. Mfadhili akatutoka. Alikuwa na ngoma 3, hana walinzi hana pa kukaa, lakini nilikuwa naye," - Jalang'o alisema.

Muhtasari

• Mbunge huyo alihadithia kwamba kipindi hicho Diamond alikuwa amealikwa kwenye shoo moja maeneo ya Pwani ya Kenya na hakuwa na mtu yeyote kama timu yake.

Jalang'o azungumzia urafiki wake na Diamond.
Jalang'o azungumzia urafiki wake na Diamond.
Image: Instagram

Mbunge wa Lang’ata Phelix Odiwuor almaarufu Jalang’o amerudisha muda nyumba na kukumbuka jinsi urafiki wake na staa mkubwa wa muziki Afrika Mashariki Diamond Platnumz ulivyoanza Zaidi ya miaka 10 iliyopita.

Katika mazungumzo na SPM Buzz wikendi iliyopita, Jalnag’o alisema kuwa alijuana na Diamond kipindi ambapo alikuwa ndio mwanzo anachipukia akiwa na nyimbo tatu tu pekee.

Mbunge huyo alihadithia kwamba kipindi hicho Diamond alikuwa amealikwa kwenye shoo moja maeneo ya Pwani ya Kenya na hakuwa na mtu yeyote kama timu yake.

Walikutana naye na baada ya tamasha, promota aliwapiga chenga na kuwaacha taabani, na hapo ndipo walijuana Zaidi na kuzidi kupalilia urafiki wao hadi leo hii.

“Diamond mara ya kwanza kukutana, tulikuwa tumeitiwa shoo Malindi. Ilikuwa inaitwa Mr na Mrs Coast…kitu kama hiyo. Mfadhili akatutoka, mimi na Diamond tukapanda Voxy mpaka Mombasa. Alikuwa na ngoma kama mbili, tatu watu walikuwa wanajua. Hiyo ni miaka mingi sana iliyopita, Zaidi ya kumi sasa, 12 hivi kama sijakosea,” Jalango alisema.

“Alikuwa na ngoma 3, hana walinzi hana pa kukaa, lakini nilikuwa naye. Hiyo siku aliniambia, siwezi sahau kitu alinifanyia katika maisha yangu. Na kutoka huo muda tumekuwa marafiki…” Jalang’o alisema huku akikataa kutaja kile ambacho msanii huyo alimfanyia ambacho hatokaa kukisahau katika maisha yake.

Mbunge huyo alisema kuwa yeye siku zote amekuwa si mtu wa kupoteza marafiki au kukaribisha utabaka kuweka mipaka baina yao, akisema kuwa anaamini sana katika urafiki kuliko kitu kingine chochote.