Mbunge Peter Salasya na Mc Jessy wakabiliana mitandaoni

Peter Salasya wameonekana wakitupiana vijembe mitandaoni na Mc Jessy baada ya mbunge huyo kujitokeza na kumsaidia mwanamuziki Stevo Simple Boy.

Muhtasari

•Hatua hii ya Peter Salasya kumsaidia Stevo haikupokelewa vyema na mchekeshaji huyo aliyegeuka na kuwa mwanasiasa kwa sababu kulingana naye alihisi haikuwa sawa kurekodi msaada wake kwa Stevo.

• Kiongozi huyo wa zamani wa chuo kikuu cha Egerton, hakuchelewa kumjibu Mc Jessy akimtaka awachane na nywele zake ambazo kulingana naye zinamgharimu pesa nyingi.

Mchekeshaji Mc Jessy na Mbunge wa Mumias Mashariki Peter Salasya.
Mchekeshaji Mc Jessy na Mbunge wa Mumias Mashariki Peter Salasya.

Mbunge wa Mumias Mashariki, Peter Salasya wameonekana wakitupiana vijembe mitandaoni na mchekeshaji Mc Jessy baada ya mbunge huyo kujitokeza na kumsaidia mwanamuziki Stevo Simple Boy.

Mbunge huyo wa mhula wa kwanza kwenye bunge la kitaifa, siku ya Jumatano alijitokeza na kumhamisha Stevo Simple Boy kutoka mtaa wa mabanda wa Kibera kumpeleka kwenye nyumba  wa kifahari.

“Nilimuuliza mke wake ‘umependa hiyo place?’.. Bibi ndiye huwa anaamua. Alisema iko juu. Nikasema kama ashasema iko juu, iko sawa nikalipa. Kila kitu kiko sawa,” Salasya alisema.

Hatua hii ya Peter Salasya kumsaidia Stevo haikupokelewa vyema na mchekeshaji huyo aliyegeuka na kuwa mwanasiasa kwa sababu kulingana naye alihisi haikuwa sawa kurekodi msaada wake kwa Stevo.

“Watu wanacheza na kumsaidia Stevo waache hio maneno kwa sababu kama unataka kumsaidia uhitaji kamera na kurekodi ukimsaidia. Kuna mbunge wa huko Mumias ambaye hachani nywele ako hapo analia anataka kumsaidia Stevo Simple Boy si ufanye na usimrekodi.”

Mc Jessy Aliongeza: “Uko kwako Mumias East mbona hutuekei vitu umefanya huko unataka kutuekea kitu umefanyia Stevo Simple Boy. ni vijana wangapi huko Mumias East umesaidia kitalanta?”

Kiongozi huyo wa zamani wa chuo kikuu cha Egerton, hakuchelewa kumjibu Mc Jessy akimtaka awachane na nywele zake ambazo kulingana naye zinamgharimu pesa nyingi.

“Nikama kuna watu wanahisi vibaya Stevo akisaidiwa, sasa sai Mc Jessy anajitokeza na kusema ati sichanangi nywele. Huyo mtu hajui hii nywele ni brand? Achana na nywele yangu ata nikikupea hii nywele siku moja huwezi imaintain ata kwa mwezi moja pekee.”

Mheshimiwa Peter Salasya aliongeza kuwa atamfunza Mc Jessy njia ya kushinda kura katika uchaguzi baada ya mchkeshaji huyo kufeli kukishinda kiti ya ubunge katika kaunti ya Meru.

“Mc Jessy wewe ulisimama kura ukaanguka na ata ukanyimwa tikiti ya chama cha UDA ukaamua kusimama kama mpinzani huru. Kuja polepole nikuonyeshe siasa alafu utakuwa mbunge.”