Hauhitaji kamera karibu ili kumpa Stevo Simple Boy msaada - MC Jessy kwa MP Salasya

"Kuna Mbunge wa Mumias yule mwenye hachani nywele, ako napo na Analia ooh tunataka kufanyia stevo hivi… si ufanye na usimrekodi! Mbona unarekodi kama kweli unataka kusaidia?” - Jessy.

Muhtasari

• "Ni achague moja ama kuwa mwanasosholaiti au mbunge. Usichukulie faida [ya kuteleza kwa ganda la ndizi] kwa msanii, kama unamsaidia msaidie tu kimya kimya,” alisema.

Amsuta vikali MP Salasya kwa kile alisema ni ku'clout chase na shida zake.
MC Jessy: Amsuta vikali MP Salasya kwa kile alisema ni ku'clout chase na shida zake.
Image: Facebook

Mchekeshaji wa muda mrefu ambaye pia aliwahi kuwa mgombea wa ubunge South Imenti, MC Jessy amemkaripia vikali mbunge wa Mumias East Peter Salasya kwa kile alisema kuwa mbunge huyo anafukuzia kiki na shida za msanii Stevo Simple Boy.

Katika mazungumzo na wanablogu wa mitandaoni, Jessy alisema kuwa mbunge huyo anajaribu kujionesha kuwa mstari wa mbele kumsaidia msanii mwenye mwenye matatizo chungu nzima, huku akisema kuwa mtu ambaye anataka kutoa msaada ule wa kweli hahitaji kamera karibu naye ili kutoa msaada.

Jessy alimkoromea Salasya vikali akimtaja kuwa mbunge ambaye hachani nywele.

“Kama ishu ya Stevo Simple Boy, watu ambao nawaona wanacheza karibu naye eti ni kumsaidia na mambo mengine wanafaa waache hayo maneno kwa sababu kama unataka kumsaidia hauhitaji kamera karibu ili kutoa msaada.  Kuna Mbunge wa Mumias yule mwenye hachani nywele, ako napo na Analia ooh tunataka kufanyia stevo hivi… si ufanye na usimrekodi! Mbona unarekodi kama kweli unataka kusaidia?” Jessy alisema kwa kughadhabika.

Jessy alisema kuwa kwa Obinna kusema alikuwa na nia ya kumsaidia Stevo inaeleweka kwa sababu yeye ni mkuza maudhui na wao hujitafutia riziki yao kule, lakini kwa mbunge huyo kidogo alihisi kuna taswishi kubwa.

“Kwa Obinna naeza elewa yeye ni msanii ni mkuza maudhui wanapata maudhui kwa njia hiyo, lakini kwa mbunge inakuwaje, mbona mbunge afanye vile? Ni achague moja ama kuwa mwanasosholaiti au mbunge. Usichukulie faida [ya kuteleza kwa ganda la ndizi] kwa msanii, kama unamsaidia msaidie tu kimya kimya,” alisema.

Hii inakuja siku moja baada ya mbunge huyo kupakia video kwenye mitandao yake ya kijamii akisema kuwa hatimaye alitimiza ahadi yake kwa familia ya msanii huyo kwa kumhamishia kwenye mazingira salama huku pia akisema kuwa hivi karibuni atamjengea nyumba ya kisasa nyumbani kwao Oyugis kaunti ya Homa Bay.

Suala la Stevo liligonga vichwa vya habari wiki mbili zilizopita baada ya mkewe Grace Atieno kufanya mahojiano na kufunguka kwamba Stevo anapitia wakati mgumu na usimamizi wake kipindi hicho MIB kwa kile alisema kuwa msanii huyo hapati chochote kitu kutokana na kazi zake za Sanaa kiasi kwamba inawabidi wanalala njaa wakati mwingine.