Chameleone apanda jukwaani na vibe kama lote siku chache baada ya kuondoka hospitalini

Mashabiki wengi walishangaa kumuona akitumbuiza jukwaani ikiwa ni siku chache tu baada ya familia yake kuvunja kimya kwamba alikuwa amelazwa na alihitajika kufanyiwa upasuaji.

Muhtasari

• Msanii huyo familia yake ilikuwa imevunja kimya kwamba walihitaji msaada wa kifedha kusimamia matibabu yake Marekani.

Atumbuiza jukwaani siku chache baada ya kuondoka hospitalini.
Jose Chameleone Atumbuiza jukwaani siku chache baada ya kuondoka hospitalini.
Image: Instagram

Mwimbaji wa Leone Island Music Empire Jose Chameleone, jina halisi Joseph Mayanja aliwashangaza wengi baada ya kujitupa mazima jukwaani siku moja tu baada ya kutangaza kuondoka hospitalini.

Katika video ambayo msanii huyo alipakia kwenye Instagram yake, alionekana akitumbuiza kwenye jukwaa katika tamasha la Afro Fest nchini Canada, ikiwa ni siku moja tu baada ya kutangazwa kuruhusiwa kuondoka hospitalini Marekani alikokuwa amelazwa na kufanyiwa upasuaji kulingana na vyanzo vya habari karibu naye.

Siku moja nyuma, Jose Chameleone aliruhusiwa kutoka Hospitali ya Aline Medical huko Minneapolis baada ya wiki za kutathminiwa na matibabu.

Kupitia akaunti zake za mitandao ya kijamii, Chameleone alionyesha imani yake ya kupona haraka, ingawa alikiri kwamba inaweza kuchukua muda na uvumilivu.

Alipokuwa akirejea katika afya yake ya kawaida, Chameleone alijitokeza kwa ujasiri na kutumbuiza mwishoni mwa juma kwenye tamasha hilo la Afro Fest huko Toronto.

Katika video, Chameleone anaweza kuonekana akitumbuiza akiwa ameketi kwenye kiti, kabla ya kwenda kwa wahudhuriaji kuwapungia mikono.

Akinukuu video yake ya uigizaji kwenye Instagram, Chameleone aliwashukuru mashabiki wake kwa upendo wao usio na masharti na kuwahakikishia utendaji mwingine mzuri na bora zaidi.

“Nilijitokeza - Asante kwa upendo usio na masharti. Tabasamu kwenye nyuso zenu ni dua kwa ajili yangu. Siku moja tutarudi kwa njia kubwa, safi na bora Zaidi,” aliandika.

“Asante kwa usimamizi kwa uangalifu wote maalum. Tutarudi msimu ujao wa joto,” aliongeza.

Afro Fest ni mojawapo ya Tamasha kubwa zaidi la bure la Muziki wa Kiafrika huko Amerika Kaskazini linalofanyika kila mwaka katika Woodbine Park - Toronto.