Akothee anusuruka shambulio la majangili waliojihami kwa panga barabarani usiku

Akothee alisema watu hao ambao hakuwajua ni kina nani walikuwa wamefunga barabara kwa mawe na walikuwa wamejihami kwa panga na silaha zingine za kutisha.

Muhtasari

• Akothee aliwatahadharisha wafuasi wake kuwa makini kwani vijana wengi wameanza kutumia fursa ya wito wa maandamano kutekeleza visa vya wizi.

Ashambuliwa na watu waliojihami kwa panga
Akothee Ashambuliwa na watu waliojihami kwa panga
Image: Facebook

Msanii wa kizazi kipya ambaye pia ni mjasiriamali Akothee ametoa tahadhari kwa mashabiki na wafuasi wake mitandaoni kuhusu visa vya ujambazi ambavyo vinatendeka katika barabara usiku humu nchini.

Akothee kupitia ukurasa wake wa Facebook aliandika ujumbe wenye ukakasi akisema kuwa alishambuliwa na watu waliokuwa wamejihami kwa panga na silaha zingine usiku katika barabara eneo la Kendu Bay.

Msanii huyo alisema kuwa majangili hao walisimamisha gari lake na walikuwa wamefunga barabara hiyo kwa mawe.

Baada ya kusimamishwa, Akothee aliingiwa na woga katika kile alikitaja kuwa karibu ajiendee haja kubwa lakini kwa bahati nzuri wakamruhusu kuondoka.

Msanii huyo aliwatahadharisha wafuasi wake kuwa makini haswa nyakati za usiku wanaposafiri kwani kuna makundi ya vijana ambao wameanzisha vurugu za kufunga barabara kwa mawe na wamejihami kwa panga na silaha zingine za kutisha.

“Hey Yeyote anayesafiri usiku wa leo aonywe. Nimepita tu kendu bay wamefunga barabara kwa mawe na kubeba panga, wameniruhusu nipite, lakini trust me, karibu nijiendee haja kubwa 🙏. Kuwa salama. Walituambia tuweke majani kwenye gari letu na kututakia safari njema 🤔💪 Sina habari walikuwa kina nani, lakini kuwa salana” Akothee alisema.

Msanii huyo pia alikumbuka kwamba wiki jana meneja wake alipoteza vitu vya muhimu ikiwemo kipakatalishi chake baada ya vijana waliojihami kwa silaha kushambulia basi alilokuwa ameabiri mchana peupe katika kaunti ya Kisii.

“Producer wangu alipoteza mali yake ikiwa ni pamoja na laptop yake yote alipokuwa akisafiri Ijumaa wiki iliyopita, basi lao lilivunjwa huko Kisii, mchana imagine,” Akothee alisema.

Baadhi walihisi hao ni vijana watoro ambao wanatumia fursa na nafasi ya wito wa maandamano na muungano wa upinzani na kuanza kutekeleza vitendo visivyo sahihi katika jamii.