Mbona JuaCali aliomba Njugush radhi kama anaamini kile alichokisema? - Nyamu ahoji

"...sasa mbona aombe msamaha kama kweli anaamini katika kile alichokisema, ama ulikuwa tu mkwara?” - Nyamu aliuliza.

Muhtasari

• Kwa upande wake, Nyamu alikiri kwamba Njugush ni mchekeshaji mzuri ambaye anajitahidi kujijenga na kujipaisha kwenye majukwaa mbalimbali kimataifa.

ashangaa mbona Jua Cali alimuomba Njugush msamaha
SENETA KAREN NYAMU ashangaa mbona Jua Cali alimuomba Njugush msamaha
Image: Instagram

Wikendi iliyopita, msanii mkongwe ambaye pia ni gwiji mwanzilishi wa muziki aina ya Genge nchini Jua Cali alitoa matamshi yaliyochukuliwa kama ya dhihaka kwa mchekeshaji Njugush kupitia mtandao wa Twitter.

Jua Cali alidhihaki shoo ya Njugush nchini Australia akisema kuwa mchekeshaji huyo si mbunifu katika ucheshi wake na kumkandia kwamba yeye si mchekeshaji stadi.

Jua Cali alipokea maoni kinzani kutoka kwa watumizi wa mitandao ya kijamii baadhi waliohisi kuwa alikosea kumdhihaki Njugush hadharani huku wengine wakionekana kukubaliana naye.

Siku moja baadae, Jua Cali aliomba msamaha wake kwa Njugush akisema kuwa watu walimuelewa vibaya na kuahidi kumfikia Njugush ana kwa ana ili kumuelezea maana yake.

Lakini seneta maalum Karen Nyamu anahisi kwamba msanii huyo mkongwe hakufaa kuomba msamaha kwa Njugush, katika kile anasema kwamba ikiwa kweli Jua Cali anaamini katika kile aichokisema basi anafaa kusimama nacho na si kunywea na kuomba radhi.

“Kwa hiyo tena Jua Cali ameomba msamaha kwa Njugush… sasa mbona aombe msamaha kama kweli anaamini katika kile alichokisema, ama ulikuwa tu mkwara?” Karen Nyamu aliuliza kupitia Insta story yake.

Kwa upande wake, Nyamu alikiri kwamba Njugush ni mchekeshaji mzuri ambaye anajitahidi kujijenga na kujipaisha kwenye majukwaa mbalimbali kimataifa, na anachokihitaji ni kuungwa mkono kutoka kwa wakenya wala si kupigwa makombo.

“Njugush anajitahidi kutengeneza na kufungua majukwaa kwa wale ambao wanamfuata. Anahitaji kuungwa mkono na sisi sote,” Nyamu alisema huku akionesha kufadhaishwa kwake na tasnia ya burudani ya humu nchini.