Sonko awakung'uta mavumbi wasanii wa Kaveve Kazoze, awapa mavazi, viatu vipya!

Vyanzo vya ndani vinadai kwamba Sonko aliwapa vijana hao mavazi mapya pamoja na hela na pia kuwaahidi kutumbuiza katika klabu yake ya Volume wikendi hii.

Muhtasari

• “Nitaendelea kusaidia vipaji vya wenyeji kote nchini kwa sababu wengi wao wanategemea talanta zao ili kuendelea kuishi,” alisema gavana huyo wa zamani wa Nairobi.

Sonko awazawadi wasanii wa kikundi cha Spider Gang
Kaveve Kazoze Sonko awazawadi wasanii wa kikundi cha Spider Gang
Image: Twitter

Kwa mara nyingine mfanyibiashara na mwanasiasa Mike Sonko ameonesha sehemu ya moyo wake wa kubondeka uguswapo na huruma baada ya kuwafikia wasanii wa kundi la Spider Gang na kuwabadilishia maisha.

Sonko alipakia picha kadhaa kwenye ukurasa wake wa Twitter akiwa na kikundi hicho maarufu kama Kaveve Kazoze na kusema kwamba aliamua kuwabadilishia maisha kwa kuwapa mavazi mapya.

Sonko pia aliwahidi kuwapa shoo ya kutumbuiza katika klabu yake ya starehe ya Volume jijini Mombasa.

“Lazima tuunge mkono wenzetu, niliwazawadia Spider Clan crew (Kaveve Kazoze) baadhi ya vitu kwa ajili ya maonyesho yao na pia kuwalipa kutumbuiza katika club volume mombasa wikendi hii ijayo,” Sonko alisema katika picha hiyo ya pamoja ambayo alipiwa na wasanii hao chipukizi.

Sonko aliahidi kuendelea kunyoosha mkono wake kwa wasanii chipukizi na kuwapa msaada ili kuhakikisha wanafikia viwango vyao sawa kwenye tasnia na kuweza kujinufaisha kutokana na talanta zao.

 “Nitaendelea kusaidia vipaji vya wenyeji kote nchini kwa sababu wengi wao wanategemea talanta zao ili kuendelea kuishi,” alisema gavana huyo wa zamani wa Nairobi.

Kaveve Kazoze ni kikundi ambacho kimetajwa kua kwa kasi Zaidi ambacho kinajumuisha ndugu wa familia moja na wanaongozwa na mrembo pekee kwa kundi hilo la wavulana kwa jina Ngesh wa Vasha.

Ngesh kwa kiasi kikubwa amechangia kuenea kwa kundi hilo baada ya kuonesha ustadi wake katika kutema mistari katika wimbo wa Kaveve Kazoze, huku mstari huo pamoja na ule wa ‘Cash Crop za Nyandarua ni waru’ ukiwafurahisha Wakenya.

Wimbo huo ambao umetoka takribani mwezi mmoja uliopita umewapa vijana hao umaarufu wa kukutana na watu kadhaa wenye ushawishi na mpaka sasa tayari umevuka watazamaji milioni mbili kwenda mbele katika jukwaa la video la YouTube.