Alikiba na Diamond wakutana kwenye 'Maparty Mfululu' amtania kwa kumuita Quavo!

“Angalau gemu imechangamka sasa. Na mashabiki waliopo wanaenjoy sasa. Usiniangushe jamani jitahidi kuitumia vyema nafasi hii," Diamond alimwambia Alikiba.

Muhtasari

• Wiki chache zilizopita Diamond alisema kuanzia Julai hii ataachia wimbo baada ya wimbo akitumia falsafa ya mvua ya mawe.

• Alikiba naye akirejelea kauli hiyo, alisema kuwa hata baada ya kuachia wimbo wa Sumu, bado Julai hajamalizana nayo kwa kutoa nyimbo.

Alikiba amfananisha na Quavo.
DIAMOND PLATNUMZ: Alikiba amfananisha na Quavo.
Image: Instagram

Baada ya muda mrefu kwa kile kinachoaminika na wengi kuwa ni bifu kali kati ya Alikiba na Diamond, hatimaye wasanii hao wawili wameonekana kutaniana mitandaoni kwa mbwembwe za mashabiki wao.

Miezi kadhaa baada ya Diamond kudokeza kwamba anapenda sana utunzi wa Alikiba haswa katika kibao cha ‘Asali’ sasa imekuwa ni zamu ya Alikiba kuutambua mchango wa mwenzake na kumsifia pakubwa.

Alikiba katika kauli yake ya hivi karibuni kwenye mtandao wa Twitter, alionekana kumsifia Diamond kwa njia ya utani hadi kufikia hatua ya kumfananisha ya rapa kutoka kundi la Migos nchini Marekani, Quavo.

Alikiba alikumbatia kauli ya Diamond kuhusu kufanya tafrija za kutangaza ngoma zake ili kusalia kwenye trend hadi Janauri mwakani, kauli ambayo anaiita ‘Maparty mfululu’ akiwa na maana kuwa ni kushiriki tamasha baada ya tamasha kwa mfululizo.

Alikiba aliikumbatia kauli hiyo na kuitaja kuwa ni ya mdogo wake – Diamond Platnumz.

“Maparty Mfululu kama asemavyo bwana mdogo ‘Kwevo’ yanaendelea,” alisema msanii huyo.

Kwa kuonesha kuzidi kuzimenya na Diamond, alikiba naye aliapa kuendelea kutesa kwa vibao moto mwaka huu akisema kwamba hii Julai badi hajamalizana nayo.

Hii 2023 ni Ngoma Mfululu!……. July bado sijamalizana nayo ….. Hii miparty mfululu itaendelea mpaka wiki ijayo,” aliandika Alikiba.

Akimjibu kupitia Instagram, Diamond alisema kuwa ni yeye amefanya tasnia ya muziki kuchangamka baada ya kula yamini kuachia kile alichokiita ‘mvua ya mawe’ kuanzia Julai hadi Januari mwakani.

Aliwataka wasanii wanaoteleza kwa ‘Maparty mfululu’ kutumia fursa hiyo vizuri na wasije wakaiacha ikapoa baada yake yeye kuichangamsha.

“Angalau gemu imechangamka sasa. Na mashabiki waliopo wanaenjoy sasa. Msiniangushe jamani jitahidi kuitumia vyema nafasi hii. Mkizembea tena kwa kweli sitatoa msaada mwingine. Maana nitachoka sasa sababu ujue mimi pia ni binadamu…” Diamond alisema.