Stevo: Mimi ni kama Diamond wa Kenya, lakini ngoma zangu ni za kuhimiza jamii

“Unajua si kila mtu huwa anataka kusikiliza ngoma za hepi moments za kusisimua mwili hapana, mle ndani kuna wazee, kuna wale watu... imbeni ngoma ambayo a unaweza kusikiliza hata na mzazi,”

Muhtasari

• “Wasanii wa Kenya watie bidii waache kuimba ngoma ambazo hazileti shangwe, waimbe ngoma amabzo zinamake sense." - Stevo.

Stevo SIple boy, adai yeye ni kama Diamond
Stevo SIple boy, adai yeye ni kama Diamond
Image: Instagram

Msanii wa kizazi kipya nchini Stevo Simple Boy amejipiga kifua akisema kwamba watu wengi humlinganisha na msanii namba moja katika ukanda wa Afrika Mashariki kutoka Tanzania, Diamond Platnuzm.

Katika mazungumzo na chaneli ya 2mbili YouTube, Stevo alisema kwamba uwezo wake katika kutunga mashauri ya muziki kwa sauti ya kumtoa nyoka pangoni siku nyingi umekuwa ukifananishwa na ule wa Diamond pika pakua.

“Najua Wakenya na watu wengine walikuwa wanasema eti mimi ni Diamond wa Kenya. Kwa hiyo mimi nilikuwa nasema hizo zikitulia naachilia ngoma, unaona.”

Msanii huyo aliwashauri wasanii wenzake wa Kenya kutunga nyimbo ambazo ni za ubora wa kipekee kuwawezesha kushiriki katika tuzo za kimataifa.

“Wasanii wa Kenya watie bidii waache kuimba ngoma ambazo hazileti shangwe, waimbe ngoma amabzo zinamake sense. Wasanii sisi tunajituma Zaidi, ukiangalia mimi kwa staili yangu na wasanii wengine tuko tofauti. Mimi sana sana napenda kuhimiza jamii ambayo ni kuwapatia ujumbe, siimbi ngoma za kupotosha watu,” alisema.

“Unajua si kila mtu huwa anataka kusikiliza ngoma za hepi moments za kusisimua mwili hapana, mle ndani kuna wazee, kuna wale watu wazima, imbeni ngoma ambayo hata ukiwa pale kwa nyumba unaweza kusikiliza hata na mzazi,” aliongeza.

Msanii huyo ambaye amepotea mitandaoni amesema kwamba bado akaunti zake za mitandao ya kijamii bado zinashikiliwa na uongozi wake wa awali ambao ulimtema pindi alipovunja ukimya kuhusu madhira yake.

Aliomba kwamba bado wanaendelea kutafuta mwafka nao akisema kuwa moja kati ya suluhu ananolitaka ni uongozi wa MIB kuchukua maokoto ya nyimbo zilizopo kwenye chaneli yake na kumrudishia chaneli aanze upya.

“Mimi ningependa kuomba hizo ngoma ambazo ziko kwa hiyo chaneli wachukue revenue lakini waniachie akaunti. Uongozi ndio ulinifungulia chaneli hiyo wakasema kama kuna makosa ambayo yatatokea watanipatia akaunti hiyo,” Stevo alifunguka.

Hivi majuzi Stivo ametishia kuwasilisha kesi mahakamani dhidi ya wakuu wake wa zamani kwa kukataa kutoa akaunti zake za mitandao ya kijamii. Kitu alichodai kimekwamisha uthabiti wake wa muziki.

Kuhusu ni kwa nini aliamua sasa hataki uongozi, Stevo alikuwa na haya ya kusema;

“Unajua mameneja wanakuja kwa upole halafu hapo katikati wanakuja kugeuka. Kwa hiyo nikasema acha nikae peke yangu ndio nione. Kama sitakuwa vizuri wakati mwingine nitahitaji meneja,” alisema akifutilia mbali uwezekano wa kutokuwa chini ya uongozi tena.