Ingekuwa muziki ni vocal Wema Sepetu angekuwa msanii mkubwa kwa hii nchi - Diamond

“Kwa mfano Burna Boy alikaa akasema ‘sauti yangu ya bass hii, naifanya hadi watu waikubali’ na ndio hivyo akaifanya na sisi wote tukaikubali. Mambo ya vocal ni ya miaka ya nyuma" - Diamond.

Muhtasari

•Diamond alisema mambo ya kufuata sauti nzuri ndio uwe msanii ni ya miaka ya zamani, akisisitiza kwamba siku hizi ni ubunifu.

• Alimsifia Wema Sepetu kwamba ingekuwa wanafuata vocals basi angekuwa msanii namba moja kwa ustadi wake wa sauti.

Diamond na Wema Sepetu.
Diamond na Wema Sepetu.
Image: Instagram

Diamond Platnumz kwa mara nyingine amepiga pale kwenye mshono kuhusu suala la Alikiba kwamba wasanii wanafaa kutafuta mafunzo ya kujua jinsi ya kupata sauti nzuri ya kuimba, kwa kimombo vocalists.

Akizungumza katika tukio kubwa la mzalishaji wa muziki S2Kizzy usiku wa Jumatatu, Diamond alisema kuwa kauli hiyo ya Alikiba kujisifia kwamba yeye ndio msanii mwenye vocals nzuri ni ya kupotosha kwani siku hizi muziki sio vocals tu bali pia ubunifu unachangia.

Diamond alisema kwamba ingekuwa kinachoangaliwa kwenye muziki ni vocals tu basi msanii mkubwa kutoka Nigeria Burna Boy asingekuwa na ukubwa ule.

Pia alisema kuwa ingekuwa muziki ungeangaliwa kutoka kwa kioo cha vocals basi mpenzi wake wa zamani, Wema Sepetu angekuwa msanii namba moja kwa nchi – kwani ndiye mwanadada mwenye sauti nzuri sana ambayo amewahi sikia.

“Ingekuwa muziki ni vocals Burna Boy sasa hivi angekuwa haimbi tena. Angekuwa ndiye msanii wa mwisho Afrika kama muziki ungekuwa ni wa kuangaliwa kwa vocals. Msanii wa kwanza angekuwa Wema Sepetu kwenye hii nchi. Unatakiwa uwe mbunifu, sauti yako Mungu alokuumba nayo unatakiuwa ujue unaitumia vipi na ndio maana nina hit nyingi sana,” Diamond alijipiga kifua.

Msanii huyo alisema kwamba kinachotakiwa ni msanii kufanya makeke yote kadri ya uwezo wake ili kujua sauti yake watu wataikubali vipi.

“Kwa mfano Burna Boy alikaa akasema ‘sauti yangu ya bass hii, naifanya hadi watu waikubali’ na ndio hivyo akaifanya na sisi wote tukaikubali. Kwa hiyo inatakiwa ubunifu, promotion, strategies. Mambo ya vocal ni ya miaka ya nyuma, sasa hivi tunahitaji una ubunifu kiasi gani, ujanja kiasi gani. Mimi naimba muziki wowote kutumia sauti, kutumia bass, kutumia rap naimba, ndio maana ya kuwa mwanamuziki, Sanaa,” Diamond alisema.

Jumatano Diamond na Alikiba walipapurana mitandaoni kisa muziki huku Alikiba akijisifia kuwa msanii mwenye vocals nzuri jambo ambalo Diamond alimkosoa vikali akisema yake si vocals bali ni kubana pua na kusema wasanii wenye vocals ni kina Barnaba Classic.