Harmonize akiri wimbo wa Diamond na Rayvanny 'Tetema' ni mkubwa, ispokuwa…

“Bado nakukumbuka jinsi walivyokuwa wakisema kwamba ni vigumu kufanya nyimbo za Kiingereza. Walisema sijui Kiingereza ili tu kuzima ndoto yangu." - Harmonize.

Muhtasari

• Harmonize alisema kuwa wimbo huo ulifanya vizuri lakini ungefika hata mbali Zaidi kama ungekuwa katika lugha ya Kiingereza.

• Harmonize alitoa changamoto kwa wanaopinga kwamba hana ustadi wa Kiingereza.

Harmonize ausifia Tetema
Harmonize ausifia Tetema
Image: Screengrab

Kwa mara ya kwanza, msanii Harmonize amekubali kwamba wimbo wa ‘Tetema’ – collabo ya Diamond na Rayvanny ya mwaka 2018 ni moja ya wimbo mkubwa sana uliowahi toka katika tasnia ya Bongo Fleva.

Harmonize kupitia Instagram Stories zake, alikiri kwamba wimbo huo ulikuwa mkubwa lakini akasema kuwa mapungufu macheche yalikuwa ni pamoja na kuwa katika lugha ya Kiswahili.

Harmonize alisema kuwa wimbo huo ulifanya vizuri lakini ungefika hata mbali Zaidi kama ungekuwa katika lugha ya Kiingereza – lugha inayochukuliwa na kukubaliwa na wengi kuwa ni lugha ya dunia.

Msanii huyo alisema kwamba baada ya kugundua mapungufu hayo, aliketi chini na kuandika wimbo wake – Single Again – ambao uko katika lugha ya Kiingereza na amesema umepata mafanikio makubwa kiasi kwamba kila aendapo anawakuta watu wanaimba neno baada ya jingine kote duniani.

“Tetema ni wimbo mkubwa Zaidi katika historia ya Tanzania. Hongera kakangu Chui [Rayvanny], lakini bado ni wimbo wa Kiswahili. Sasa hebu tuzungumzie nyimbo za Kiingereza. Mimi ni jamaa aliyebarikiwa huku nje,” Harmonize alisema.

Msanii huyo alizidi kuelezea jinsi alivyopatana na ugumu wakati alitoa wazo la kuandika nyimbo kwa Kiingereza, lakini kwa kuangalia nyuma, Harmonize anasema juhudi zake zimezaa matunda na sasa kwa mikogo anaweza tamba kuwa msanii wa kwanza kutoka Tanzania mwenye ustadi wa hali ya juu katika kuandika mashairi ya Kiingereza.

“Bado nakukumbuka jinsi walivyokuwa wakisema kwamba ni vigumu kufanya nyimbo za Kiingereza. Walisema sijui Kiingereza ili tu kuzima ndoto yangu. Lol. Endelea kusonga mbele kwa sababu hakuna mwingine kama wewe, kwenye maisha ni kuhusu wewe na Mungu. Mimi ndio msanii bora wa East Africa katika kuandika nyimbo za Kiingereza,” alisema.

Harmonize alitoa changamoto kwa wanaopinga kwamba hana ustadi wa Kiingereza. Alisema kwamba mtu yeyote akimtumia video ya msanii wa Bongo akitumbuiza wimbo wa kiingereza na umati unaimba naye neno baada ya jingine basi atampa zawadi ya kitita cha hela.

“Unaweza shiriki video ya msanii wako pendwa East Africa akiwa anafanya shoo na watu wanaimba wimbo wake wa Kiingereza neno baada ya neno na utajishindia shilingi milioni 100. Hili shindano litakwenda mpaka 2030, chukua muda wako,” Harmonize alitema tambo.