Baada ya kusema naondoka, Harmonize alinipokonya gari alilonipa kama zawadi - Jabulant

“Swali la gari nitajibu jinsi lilivyo sitaficha kuwa hawajachukua itakuwa imeniumiza kuficha kitu ambacho kipo wazi,” alimaliza.

Muhtasari

• Alisema jambo hilo halimuumizi kwa njia yoyote maana alishajipanga mapema kwa kununua gari la kwake.

• Jabulant alitetea uamuzi wake wa kufunguka ukweli ili kuutenga na uongo.

Jablant na aliyekuwa bosi wake Harmonize.
Jablant na aliyekuwa bosi wake Harmonize.
Image: Instagram

Aliyekuwa mpiga picha wa msanii Harmonize, Jabulant kwa mara ya kwanza amefunguka kwamba baada ya kutangaza kwamba anaondoka kwenye lebo ya Konde Gang, uongozi huo ulichukua gari ambalo walikuwa wamempa siku za nyuma kama zawadi ya kazi nzuri.

Jabulant alifunguka haya wakati aliwapa mashabiki wake nafasi ya kumuuliza maswali kwenye kipindi cha maswali na majibu cha Instagram.

Mmoja alimtaka kunyoosha maelezo kuhusu uvumi kwamba alipokonywa gari na Jabulant aliandika jibu refu akieleza jinsi alinyanganywa gari hilo na baya Zaidi alisema alichukia mazingira ambayo gari hilo lilichukuliwa kwa dharau kubwa.

“Ni kweli gari hilo aina ya Vitz walinipa kama zawadi name nililichukulia kama zawadi ya kazi yangu lakini sio uongo ni kweli gari lilichukuliwa tena kinachoniuma Zaidi ni namna ambavyo walitumia njia ndefu kulichukua gari hilo,” alianza Jabulant.

Jabulant alitetea uamuzi wake wa kufunguka ukweli ili kuutenga na uongo akisema kwamba kwa kunyosha maelezo, alikuwa anatengeneza mazingira kuwa sawa kwa kuepuka maswali ya mara kwa mara.

Alisema jambo hilo halimuumizi kwa njia yoyote maana alishajipanga mapema kwa kununua gari la kwake.

“Ni lazima niongee kwa sababu waliponipa walipost taarifa hiyo na hivyo hata hili walipochukua gari ilifaa waposti ili nisiwe naulizwa maswali kuhusu hilo gari. Lazima niongee sababu sio  kitu cha kuficha na sio kama inaniumiza, hapana. Mimi nilishanunua gari langu kitambo tu kabla hata sijatoka kwenye kundi,” alisema.

“Swali la gari nitajibu jinsi lilivyo sitaficha kuwa hawajachukua itakuwa imeniumiza kuficha kitu ambacho kipo wazi,” alimaliza.

Huyu sio mtu wa kwanza kuondoka Konde Gang na baadae kudai kuvuliwa umiliki wa baadhi ya vitu alivyopewa akiwa pale.

Unakumbuka pia wasanii Country Boy na Anjella baada ya kuondoka waliweka wazi kwamba magari ambayo walikuwa wanayatumia wakati wako chini ya Konde Music Worldwide yalichukuliwa pindi baada ya mikataba yao kuchanwa.