Rapa Breeder LW afafanua mbona anahisi Diana Marua ni msanii mzuri wa rap

Breeder alisema kwamba Diana Marua ni mtu ambaye ana ujasiri wa kiwango cha juu sana, kitu ambacho alisema ndio huleta mafanikio makubwa kwa wasanii haswa wale wa kike.

Muhtasari

• Breeder alifichua kwamba alikuwa ameandika diss track 6 kwa ajili ya wenzao wa Tanzania lakini alitoa 2 tu.

Diana Marua na Breeder LW.
Diana Marua na Breeder LW.
Image: Insta

Msanii wa HipHop nchini Kenya, Breeder LW ametetea hatua yake ya kumtaja mwanablogu ambaye pia ni msanii wa rap Diana Marua kama mmoja wa wasanii wa kike wanaofanya vizuri na kuleta mbwembwe katika Sanaa ya hiphop Kenya.

Siku chache zilizopita Breeder katika mahojiano alimtaja Diana Marua kuwa miongoni mwa wasanii wazuri wa muziki wa rap japo baadhi ya mashabiki wake walihisi kwamba anambeba kwa mbeleko lakini rapa huyo sasa amejitokeza na kutetea au kufafanua mbona anahisi Diana Marua ni mzuri katika kurap.

Breeder alisema kwamba Diana Marua ni mtu ambaye ana ujasiri wa kiwango cha juu sana, kitu ambacho alisema ndio huleta mafanikio makubwa kwa wasanii haswa wale wa kike.

“Diana B kwanza ako na ujasiri ambacho ni kitu cha maana sana. Unajua mtu unaweza kuwa mzuri Zaidi kuliko jirani yako lakini je, unajiamini mwenyewe? Una ujasiri wa kushika kipaza sauti, kuchukua beat na kurap vitu unarap. Mimi natambua sana mtu ambaye anajiamini. Yeye kuwa na huo ujasiri na kusema kwamba hajali chenye watu watasema kumhusu, naheshimu huo moyo sana,” Breeder LW alisema.

Rapa huyo ambaye alimiminiwa sifa na rapa nguli Khaligraph Jones alisema kwamba katika kipindi ambacho amekuwa kwenye Sanaa ya muziki, amekutana na wasanii wengi chipukizi ambao ni wazuri lakini ambao wanashindwa kufika kiwango kingine kwa kutojiamini.

“Diana B ni msanii mzuri kwa sababu anajitambua na mwisho wa siku anachukua beat na kutema mistari,” Breeder aliongeza.

Akizungumzia bifu ambalo lilioteshwa wiki chache zilizopita na Khaligraph kati ya wasanii wa rap wa Kenya na Tanzania, Breeder ambaye alitoa diss track mbili kuwatumbia makombo wenzao wa Tanzania alifichua kwamba alikuwa ameshaandika diss tracks 6 lakini hakuweza kuzitoa zote kwa sababu aliona wenzao wa Tanzania wameshaingia tumbo maji.