'Ni njaa inakusumbua!' - Akothee amjibu KK Mwenyewe kutaka kuwa mpenzi wake

"Pata pasipoti kwanza kabla ya kubeba mabango yasiyo na maana, nataka kuoa Akothee, na nini chako? Unataka kuolewa na Akothee au unataka kuasiliwa na AKOTHEE, ni njaa ama mapenzi nkt,” Akothee.

Muhtasari

• “Madam boss Akothee niko tayari kuwa mpenzi wako wa 8. Nimechoka kunyamaza, nataka kuwa mpenzi wako na sitakuangusha,” bango hilo lilisoma.

Akothee amjibu KK Mwenyewe kutaka kumuoa
Akothee amjibu KK Mwenyewe kutaka kumuoa
Image: Insta

Siku moja baada ya mchekeshaji KK Mwenyewe kuonekana na bango la kutaka kuchukua nafasi ya Denis Schweizer maarufu Omosh kwenye maisha ya Akothee kama mpenzi, msanii huyo mwenye tambo kali amemjibu kwa shombo.

Akothee alisema kwamba watu wengi wameanza kumfanyia mzaha wakidhani kwamba yeye anaokota tu mtu yeyote na kumfanya kuwa mpenzi wake.

Alimtaka KK Mwenyewe kabla ya kutaka kuwa mpenzi wake, kwanza ahakikishe ametafuta na kupata pasipoti ya usafiri na pili kunyoosha maelezo yake kama anataka kumuoa Akothee, au Akothee kumuoa yeye au kumuasili kama mtoto wake wa kufikia.

Msanii huyo ambaye pia ni mjasiriamali alisema kwamba watu wengi ambao wamekuwa wakimhusisha Omosh kuwa raia wa Pakistan aliyeokotwa na Akothee kumesababisha hadi watu wasio na hadhi kufikiria kwamba yeye ni wa kuokota mtu yeyote.

“Jambo hili la Pakistani limewafanya Chokora wafikiri Akothee ni Mistry Nilikutana na Omosh Uswizi, kwa hivyo pata pasipoti kwanza kabla ya kubeba mabango hayo yasiyo na maana, nataka kuoa Akothee, na nini chako? Unataka kuolewa na Akothee au unataka kuasiliwa na AKOTHEE, ni njaa ama mapenzi nkt,” Akothee alisema katika aya ndefu.

Katika bango lake Jumanne, KK Mwenyewe aliandika kwamba anataka kuwa mpenzi wa 8 wa Akothee akisema kwamba amechoka kunyamazia na asingependa kunyamaza wakati ameona nafasi imejitokeza baada ya Akothee kutangaza kuwa wameachana na Mr Omosh wake.

“Madam boss Akothee niko tayari kuwa mpenzi wako wa 8. Nimechoka kunyamaza, nataka kuwa mpenzi wako na sitakuangusha,” bango hilo lilisoma.

Ndoa ya kifahari ya Akothee na Omosh ilifanyika mwezi Aprili mwaka huu lakini haikudumu kuonesha maana ya hadhi hiyo kwani chini ya miezi 4 tu msanii huyo alitangaza kwamba alichokiona nchini Uswizi ni cha kusimuliwa siku nyingine, ikiwa ni baada ya wiki kadhaa kuwajibu kwa ukali mashabiki waliokuwa wakitaka kujua kuhusu uwepo wa Omosh aliyekosekana katika picha za pamoja na Akothee kwa muda.