Kimani Mbugua anunua kamera na vifaa vya video kwa Sh 500,000 alizopokea kwa mchango

Alieleza kwamba ametumia pesa hizo kwa njia mwafaka kwa kununua vifaa ambavyo vitamwezesha kuendeleza shughuli zake za mawasiliano.

Muhtasari

•"Nataka kurudi kwako na kusema asante kwa usaidizi wote na upendo wenu, haswa hapa kwenye TikTok,"

Kimani Mbugua/Instagram
Kimani Mbugua/Instagram

Aliyekuwa mtangazaji, Kimani Mbugua ameelezea furaha aliyonayo baada ya kununua kamera na vifaa vya  video kupitia mchango aliopokea kutoka kwa wasamaria wema.

Kupitia video aliyopakia kwenye ukurasa wake wa TikTok, alichukua fursa hiyo kuwashukuru wakenya wote ambao walisimama na yeye wakati alipokuwa akipitia hali ngumu hivi karibuni.

"Nataka kurudi kwako na kusema asante kwa usaidizi wote na upendo wenu, haswa hapa kwenye TikTok," alisema.

Alieleza kwamba ametumia pesa hizo kwa njia mwafaka kwa kununua vifaa ambavyo vitamwezesha kuendeleza shughuli zake za mawasiliano.

"Nimefurahi sana, unaweza kuona usoni mwangu, nina furaha sana, na nilitaka tu kusema asante kwa kila mmoja wenu aliyenipa kiasi chochote cha pesa alichofanikiwa nacho." aliongeza.

Mbugua alieleza jinsi alivyotumia sehemu ya fedha hizo kupata vifaa vipya vya  kuchukua video, pamoja na vipaza sauti.

Akiwa na hali ya msisimko, Mbugua alitangaza kurejea mtaani ili kuanza kufanya kazi  ambayo anasema anafurahi kuifanya.

Mbugua alisema kwamba kazi yake atainzia  pale mitaani kwao nyumbani alipokulia.

"Niko hapa nyumbani, Thika, Makongeni ni mahali pangu, hapa ndipo nilipokulia, kwa hivyo narudi hapa kama mwanahabari,” aliongeza Mbugua.

Kulingana na Mbugua, atakuwa akiwahoji watu katika mitaa ya Thika huku akifanya mambo mengine mitaani.

"Kufurahiya kama tunavyofanya kila wakati, kwa hivyo angalia, inakuja hivi karibuni, lakini kwa sasa, nilitaka kusema asante sana kwa kila mtu aliyechangisha pesa," alisema.

Hivi ,majuzi muunda maudhui maarufu Nyako alifanya mchango kupitia ukurasa wake wa TikTik Live,wa kumsaidia Mbugua kujikimu kimaisha,ambapo mashabiki wake Nyako waliweza kuchanga takriban sh 500,000.

Jambo la kufurahisha zaidi ni kwamba pesa hizo zilikusanywa kwa saa moja na nusu,kuonyesha jinsi watu walikuwa wamejitolea kumpa sapoti.