Mimi ni mfano bora kwa wanawake wengi Ulaya - Akothee atamba na picha za kisichana

Akothee alisema kwamba ni wanawake wachache sana wanaoweza kuwalea na kuwaelimisha watoto 5 bila baba na kuwafanikisha watatu kati yao kuwa na makazi yao Ulaya.

Muhtasari

• Mama huyo wa watoto 5 alisema kwamba si rahisi kupata mwanamke kama yeye ambaye amewalea watoto 5 bila mume akiwa hana hata chembe ya madeni wala mikopo.

Akothee.
Akothee.
Image: Facebook

Mjasiriamali na msanii Akothee ameendelea kuwamezesha vidonge vyao wenye gere kwa kushiriki picha zake za kisichana ambazo kila sekunde iendayo kwa Mungu anazidi kuwa mbichi licha ya umri kusonga.

Msanii huyo bila kufumba jicho, alidai waziwazi kwamba yeye ni himizo kubwa sana kwa wanawake wengi katika bara la Ulaya lakini wengi humu nchini hawataki kukubali hilo kwani wanaonea gere mafanikio yake.

Mama huyo wa watoto 5 alisema kwamba si rahisi kupata mwanamke kama yeye ambaye amewalea watoto 5 bila mume akiwa hana hata chembe ya madeni wala mikopo.

“Mimi ni himizo kubwa kwa wanawake wengi barani Ulaya, kubali tu. Mama wa watoto watano aliye na Mikopo sifuri, bila kodi, kulea watoto kwa ufanisi katika familia isiyo na kazi. Watoto 3 wahitimu, Na ukaazi wa ulaya, hatuwezi kamwe kukaa kwenye meza moja. Ni viwango rafiki yangu,” Akothee alitamba.

Msanii huyo ambaye licha ya kuachwa na mpenzi wake Mr Omosh hivi karibuni alionesha kutokata tamaa ya mapenzi, alijitangaza kwamba yeye ndiye dhahabu ya Kenya, akiwapa wanaomuonea gere kwa mafanikio yake kumtajia mwanamke ambaye amewaelimisha wanawe 5 nchini pasi na kuwepo kwa baba.

“Mimi ni The Kenyan Gold sawa 🙏 Je umelea watoto wako kenya wapi. Kila kitu cha kufanya na elimu ni pesa? By the way, niwaambie wakenya 🤣🤣🤣 Elimu kwa watoto wanaozaliwa ulaya ni bure. Na hakuna hata Uniform 🤣🤣🤣. Ndio maana chawa inawamaliza, mara shule zimefungwa sijui kunguni,” alisema.

Akothee ambaye anazidi kung’ara baada ya penzi lake kuingia mitini licha ya kuwekeza pakubwa katika harusi ya kifahari takribani miezi 5 iliyopita aliwashauri watu kuishi maisha yake pasi na kutiwa presha za kijinga kwani maisha ni kama jeneza, mtu ukiwa ndani huwezi jigeuza.

“Maisha ni kama Jeneza hakuna kugeuka, sijataja mtu mimi. Ishi maisha yako mama, Asikutie mtu wasiwasi,” alisema kwa lugha ya mafamba kama alikuwa anamzomea mtu fiche.