Sikuja duniani kuteseka - Diana Marua ajigamba Bahati 'akimchafua' na pesa nyingi

"Babe, @BahatiKenya unapoendelea kunipa zawadi, tafadhali zingatia Sanduku 7 zilizofungwa zilizo na pesa ndani yake. Ni hayo tu,” Diana alimkumbusha Bahati.

Muhtasari

• Wanandoa hao wanasherehehea miaka 7 ya uhusiano na Bahati aliahidi kumpa mkewe zawadi 7 katika siku 7.

Diana Marua akioshwa na pesa na Bahati.
Diana Marua akioshwa na pesa na Bahati.
Image: Instagram

YouTuber Diana Marua ni mmoja kati ya wanawake wachache ambao wanafurahia ndoa yao hadharani kwa mapenzi ya moto kutoka kwa mume wake Bahati Kioko.

Huku wanandoa hao wakiendelea na mwendelezo wa kusherehekea miaka 7 ya mahusiano kwa Bahati kumpa Diana zawadi 7 kwa siku 7 tofauti, wamepeleka mapenzi yao katika kiwango kingine  baada ya Bahati kuandaa tafrija ya kummwagia mkewe pesa taslimu.

Diana alipakia klipu ya Bahati akimtupia pesa huku akicheza densi na kusema kwamba mumewe anajua kile ambacho hutia tabasamu kwenye uso wake, huku pia akisema kwamba katu hakuja duniani kuteseka.

“Sikuja katika ulimwengu huu kuteseka na Mume wangu anaelewa mgawo wake wa kimungu maishani mwangu, wa kunifanya niwe na Furaha kwa gharama yoyote ile,” Diana Marua aliandika kwa furaha.

Aliradidi maneno ya mumewe juzi kwamba njia pekee ya kumfanya afurahi ni kumpa pesa.

“Pesa Hunifurahisha 💃🏻 Siwezi kungoja Zawadi ya Kesho 🤩 Babe, @BahatiKenya unapoendelea kunipa zawadi, tafadhali zingatia Sanduku 7 zilizofungwa zilizo na pesa ndani yake. Ni hayo tu,” Diana alimkumbusha Bahati.

Wikendi iliyopita, Bahati alipokuwa anampa Diana zawadi ya tatu ambayo ilikuwa ni marashi ghali yaliyoagizwa kutoka Dubai, alisema kwamba yeye anamuelewa fika mpenzi wake kwamba pesa ndio lugha pekee inayomfurahia na kuyeyusha moyo wake.

“Kwa wale ambao hawajui ni vipi namfurahisha mke wangu, huwa namfanyia mambo matatu tu, moja ni kumpa hela, pili ni kumpa hela nyingi na tatu ni kumuongezea hela nyingi zaidi,” Bahati aliandika.

Hata hivyo, video hiyo ya Bahati akimtupia Diana hela ilipokelewa kwa njia mbali mbali na mashabiki wake ambao wengine walihisi ni vitimbi tu vya kuigiza huku wengine wakiwaomba wanandoa hao msaada wa kifedha, kwa kuwa walionekana wanazo nyingi za kuchezea.