Pasta Stevo Simple Boy? Msanii atokea na luku ya kutamanisha, atania kuanzisha kanisa

Msanii huyo hata hivyo kwa njia ya utani alimtaka muumini mmoja kujitolea ili kumnunulia viatu ili kuukamilisha muonekano wa suti yake.

Muhtasari

• "Naitwa mtumishi @stevosimpleboy8 sasa Sahi mkuje kwa church niwaombe na msisahau kubeba sadaka mtumishi anunue viatu." alisema.

Stevo Simple Boy
Stevo Simple Boy
Image: Instagram

Msanii Stevo Simple Boy baada ya kupata mwamko mpya, shukrani kwa Wakenya wenye moyo wa kusaidia waliojitolea kumpa shavu wakati mkewe alifichua kuwa wanapitia hali ngumu ya kimaisha, sasa amerejea mitandaoni kwa muonekano ghali.

Msanii huyo kupitia ukurasa wake wa Instagram aliorejeshewa na uongozi wake wa zamani baada ya siku kadhaa za kusukumana kuhusu umiliki wa akaunti zake, alipakia picha akiwa amevaa suti iliyompa muonekano wa kutamanisha.

Stevo kwa utani wake, alizua tambo kwamba kwa suti hiyo, tayari amefuzu moja kwa moja kuwa mhubiri, na kutania kwamba tayari amefungua kanisa na alihitaji muumini mmoja kujitolea kumnunulia viatu ili kumalizia muonekano wake.

HUNA CHAKO HUNA naitwa mtumishi @stevosimpleboy8 sasa Sahi mkuje kwa church niwaombe na msisahau kubeba sadaka mtumishi anunue viatu. SIMPLE BOY MINISTRY,” aliandika kwa utani.

Mashabiki wake wengi walifurahi kumuona akiwa na tabasamu, ikiwa ni miezi michache baada ya mkewe Grace Atieno kufichua kwa vyombo vya habari kwamba mumewe alikuwa anapitia wakati mgumu kwenye taaluma yake ya muziki, kwani uongozi wa zamani haukuwa unamchukulia kama msanii.

Grace katika kile kinaweza tajwa kuwa ulikuwa ndio mwanzo wa nuru ya Stevo, alifichua kwamba wakati mwingine Stevo anaweza itiwa shoo anaenda anatumbuiza lakini bado anarejea nyumbani wanalala njaa pasi na kitu.

Taarifa hiyo ilimfanya mbunge wa Mumias East Peter Salasya kujitolea kumpa msaada Stevo ikiwa ni pamoja na kumhamisha kwenda mazingira yenye hadhi nzuri jijini, kumlipia kodi ya miezi kadhaa, kumfungulia biashara na pia kuahidi kumjengea nyumba kijijini.