Stevo Simple Boy ammezea mate Kajala Masanja, amtongoza kwa kujitolea kumnunulia shamba

Stevo amesema amekusanya pesa za kutosha kumnunulia muigizaji huyo kipande cha ardhi nchini Kenya.

Muhtasari

•Stevo Simple Boy ameleza nia yake ya kumzawadi mpenzi huyo wa zamani wa Harmonize na kipande cha ardhi.

•“Unapenda dame unanunua maua, kiasi hicho ndiye anakuua. Nimechoka sana nipe namba ya Kajala,” aliimba

amejitolea kumnunulia shamba Kajala Masanja
Stevo Simple Boy amejitolea kumnunulia shamba Kajala Masanja
Image: INSTAGRAM

Rapa wa Kenya, Stephen Otieno Adera almaarufu Stevo Simple Boy ameonyesha kuvutiwa kwake na muigizaji mkongwe wa filamu bongo Frida Kajala Masanja.

Wakati akiifanyia matangazo kampuni ya kuuza mashamba kupitia akaunti zake za mitandao ya kijamii, mwimbaji huyo wa kibao ‘Mihadarati’ alieleza nia yake ya kumzawadi mpenzi huyo wa zamani wa Harmonize na kipande cha ardhi.

Mwimbaji huyo alidai kuwa amekusanya pesa za kutosha kumnunulia muigizaji huyo mwenye umri wa miaka 40 kipande cha ardhi nchini Kenya.

“Nimepata kitu kidogo nataka nichukulie @Kajalafrida shamba,” Stevo aliandika chini ya picha ya Kajala ambayo alichapisha.

Mwimbaji huyo aliambatanisha picha ya muigizaji huyo na mstari wa wimbo ambao aliimba hivi karibuni akiomba nambari yake.

“Unapenda dame unanunua maua, kiasi hicho ndiye anakuua. Nimechoka sana nipe namba ya Kajala,” aliimba kwenye wimbo huo.

Katika kipindi cha wiki kadhaa zilizopita, Stevo ameonyesha kuvutiwa na wasanii kadhaa wa kike akiwemo Wanja Kihii na Ngesh wa Vasha wa ‘Kaveve Kazoze.’

Mwezi jana, Ngesh ambaye amevuma sana kutokana na wimbo wao 'Kaveve Kazoze' alikataa waziwazi ombi la SStevo kuwa mpenzi wake.

Stevo alikuwa ametengeneza klipu ya video ambayo alitumia kukikiri mapenzi yake mazito kwa mwimbaji huyo mwenzake na akaendelea kumwomba awe mchumba wake ikiwa hayuko kwenye mahusiano kwa sasa.

Mwimbaji huyo wa kibao ‘Mihadarati’ aliwaomba Wakenya wamsaidie kufikisha ombi lake tamu kwa Ngesh ili kuushinda moyo wake.

“Huyu ni Stevo Simple Boy, Mondi wa Kenya maze. Kuna mwanadada pale nimeona amenivutia sana, anaitwa Kaveve Kazoze. Kama ako single, mwambie Stevo Simple Boy, mzee wa matulinga namtamani,” Stevo alisema kwenye video hiyo.

“Mfikishieni ripoti mwambie Stevo Simple Boy nimeleta kwake, wangu lazizi, wangu habibi, kwake sitamsuta nitakuwa nay eye au sio na mambo yako freshi. Aje na awe mchumba wangu, na mambo iwe freshi,” aliongeza kabla ya kutuma busu moto kwa msanii huyo wa kundi la Spider Clan.

Katika mahojiano ya simu na kituo cha redio cha humu nchini, Ngesh hata hivyo alikataa ombi la Stevo na kuweka wazi kwamba hamtaki.

Aliongeza, “Sijona video, nimeona mapicha tu natumiwa mimi sijaona video. Mimi namtaka aje sasa? Mimi nasema ata video sijaona, Achana na yeye,” Ngesh alisema.

Malkia huyo wa muziki kutoka kaunti ya Nyandarua alifichua kuwa tayari yuko kwenye mahusiano thabiti na mwanamume asiyetambulishwa na akadokeza kuwa hana nia ya kutafuta mwanamume mwingine.

“Mimi niko na mtu. Hiyo ni noma. Mimi sikuwangi na 2nd thought. Usijali mpenzi wangu anaitwa,” alisema Ngesh.