"Nyie Wakristo?" Alikiba ashindwa kujizuia, apandwa na mori katika mazishi ya msanii Haitham Kim

Wanahabari walifurika kuchukua picha na video za Alikiba akiomboleza, jambo ambalo alionekana kutolipenda.

Muhtasari

•Alikiba alishindwa kujizuia tena na ghafla akawafokea waandishi hao wa habari akiwauliza kama wao ni Wakristo.

•Baadaye alionekana akimfariji mume wa marehemu , Niite Boshen baada ya mwili wake kushushwa kwenye kaburi na kuzikwa.

katika mazishi ya Haitham Kim mnamo Septemba 2, 2023.
Alikiba katika mazishi ya Haitham Kim mnamo Septemba 2, 2023.
Image: HISANI

Staa wa Bongo, Ali Saleh Kiba almaarufu Ali Kiba alipandwa na mori wakati alipohudhuria mazishi ya marehemu malkia wa bongo fleva Haitham Kim kwenye makaburi ya Kisutu  siku ya Jumamosi.

Bosi huyo wa Kings Music alijitokeza makaburini hayo akiwa amevalia t-shirt na suruali ya jeans na kama kawaida na mastaa wengine, waandishi wa habari walifurika kuchukua picha na video zake, jambo ambalo alionekana kutolipenda.

Baada ya kukusanya hasira zake kwa muda mrefu, Kiba ambaye alionekana mwenye hisia nzito wakati wa mazishi hayo alishindwa kujizuia tena na ghafla akawafokea waandishi hao wa habari akiwauliza kama wao ni Wakristo.

“Nyie Wakristo nyie?” Alikiba kwa hasira aliwafokea waandishi hao wa habari kabla ya kuendelea kufuatilia mazishi hayo.

Staa huyo wa bongo ambaye alikuwa rafiki wa karibu wa marehemu Haitham Kim baadaye alionekana akimfariji mume wa marehemu , Niite Boshen baada ya mwili wake kushushwa kwenye kaburi na kuzikwa.

Kim ambaye katika siku za hivi majuzi alikuwa akipokea matibabu maalum baada ya kupata matatizo ya kupumua aliaga dunia katika hospitali ya Rufaa ya Temeke jijini Dar es Salaam, mwendo wa saa sita mchana siku ya Ijumaa.

Marehemu alimuacha nyuma mpenzi wake Niite Boshen na mtoto mmoja mdogo.

Kifo chake kilitokea siku chache tu baada ya wasanii wa Bongo kuanzisha kampeni ya kuchangisha pesa kwa ajili ya matibabu yake ya gharama.

Iliripotiwa kuwa marehemu alikuwa amekumbwa na matatizo ya kupumua ambapo ilianza kama homa ya kawaida lakini baadaye akawa anakosa pumzi hadi kulazwa.

Mashabiki, marafiki, wanafamilia na watu wengine wa karibu walijitokeza kumuomboleza mwimbaji na mwandishi huyo wa nyimbo.Wasanii wengi wa Bongo wakiwemo Nandy, Lukamba Harmonize, Zuchu, Kajala Masanja, Hamisa Mobetto,Wema Sepetu ni miongoni mwa wasanii ambao pia wamemuomboleza mama huyo wa mtoto mmoja.