"Sijui kilichotokea, bado tunajaribu!" Akothee amkumbuka kwa hisia mtoto aliyepoteza akiwa tumboni

Akothee alikiri kuwa bado hawajui kilichotokea hadi akapoteza ujauzito lakini akafichua bado wanaendelea kujaribu tena.

Muhtasari

•Akothee alimkumbuka kihisia ambaye angekuwa mtoto wake wa sita baada ya kukutana na familia yake ya karibu nchini Uswidi.

•Akothee alitangaza kuharibika kwa mimba ya ambaye angekuwa mtoto wake wa sita Disemba mwaka jana.

Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwimbaji na mjasiriamali wa Kenya Esther Akoth almaarufu Akothee mnamo siku ya Jumamosi alimkumbuka kihisia ambaye angekuwa mtoto wake wa sita baada ya kukutana na familia yake ya karibu nchini Uswidi.

Katika ukurasa wake wa Instagram, mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 43 ambaye kwa sasa yuko katika nchi hiyo ya Ulaya alchapisha video ya kihisia iliyomuonyesha akiwa amemshika mtoto mchanga akijaribu kumtuliza huku akiendelea kushiriki mazungumzo na mama wa mtoto huyo.

Katika taarifa yake, alisema mtoto huyo mdogo alimkumbusha ambaye angekuwa mtoto wake na mumewe Denis ‘Omosh’ Shweizer ambaye alitarajia kujifungua mwezi Julai lakini kwa bahati mbaya akapoteza ujauzito huo Desemba mwaka jana.

“Huyu mtoto amenikumbusha kuwa mtoto wetu angekuwa na mwezi 1 na wiki moja leo. Ilinibidi nimkumbushe mume wangu siku yetu kubwa tarehe 22 Julai,” Akothee alisema.

Wakati huo huo, alikiri kuwa bado hawajui kilichotokea hadi akapoteza ujauzito huo lakini akafichua kuwa bado wanaendelea kujaribu tena.

"Sijui kilichotokea, bado tunajaribu," alisema.

Katika video hiyo ambayo alichapisha, mama huyo wa watoto watano alionekana mwenye furaha na hisia nyingi huku akimshika mtoto huyo kwa uangalifu mikononi mwake.

“Hongera kwa kina mama wote wapya,” alisema.

Mwishoni mwa mwezi Mei mwaka huu wakati akimsherehekea mume wake mnamo siku yake ya kuzaliwa, Akothee alimhakikishia mzungu huyo kutoka Uswizi kuwa watapata mtoto wao pamoja hivi karibuni.

"Nina furaha sana kuanza safari mpya. Mister Omosh ungeweza kuwa baba tarehe 22 Julai 2023 lakini ya ulimwengu hutokea na tutakuwa wazazi tena hivi karibuni mpenzi wangu. Niruhusu nikutakie kheri njema. Kheri ya siku ya kuzaliwa mfalme wa umalkia wangu. Heri ya siku ya kuzaliwa  Omondi wa saba," alisema.

Awali mwezi huo, msanii huyo mwenye umri wa miaka 43 alikuwa amedokeza  kuwa ameanza maandalizi ya safari yake ya ujauzito.

Mama huyo wa watoto watano kupitia ukurasa wake wa Instagram alionyesha pakiti ya dawa aina ya Pregnacare Plus Omega-3 ambayo kwa kawaida hutumiwa na wanawake wakati wa safari ya ujauzito.

"Yoooo safari inaanza sasa NDILAS," Akothee alisema chini ya video fupi ya dawa hizo ambayo alichapisha.

Akothee alitangaza kuharibika kwa mimba ya ambaye angekuwa mtoto wake wa sita Disemba mwaka jana na kusema kwamba hali hiyoililetwa na matatizo ya ujauzito.